Na mwandishi wetu
Kuelekea mchezo wa kesho Jumamosi wa wababe wa soka, Simba dhidi ya Yanga, makocha wa timu hizo wamesema wako tayari kwa ajili ya mtanange huo huku wakijnasibu kujiandaa vyema kimbinu ili kupata matokeo.
Makocha hao wamezungumza hayo leo Ijumaa kuelekea mchezo huo utakaopigwa kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam huku Yanga ikiwa kinara kwa pointi 55 kwa mechi 21 huku Simba ikiwa ni ya tatu ikikusanya pointi 46 baada ya mechi 20.
Kocha msaidizi Simba, Selemani Matola alisema: “Haiwezi kuwa mechi rahisi kama ni ‘derby’, tunafahamu ni mchezo mgumu na Simba tunawaheshimu Yanga, wamekuwa na fomu nzuri, matokeo mazuri, kwa hiyo sisi benchi na wachezaji tunalielewa hilo na pamoja na uzuri wao na fomu yao tumejiandaa kukabiliana nao kuhakikisha tunapata matokeo hiyo kesho.”
Naye kocha mkuu wa Yanga, Miguel Gamondi alisema kuwa mchezo huo ni mgumu na anajua wapinzani wao wanataka wacheze ili washinde mechi na kulipa kisasi lakini wao wamejiandaa na kwa hilo wakifahamu wana timu imara ambayo inaweza kucheza kwenye presha ya aina yoyote, hivyo anaamini kama Wekundu hao watakuwa na mpango huo inaweza kuwagharimu pia.

Timu hizo za Mitaa ya Kariakoo, zinashuka dimbani zikiwa na kumbukumbu ya Simba kupoteza kwa mabao 5-1 katika mchezo wa mwisho walipokutana kwenye ligi Novemba 5, mwaka jana.
Mbali na hilo, mchezo huo umeteka pia hisia za wengi kutokana na kuwa ni miongoni mwa mechi zitakazotoa taswira ya ubingwa mpaka sasa zikiwa zimesalia mechi saba kabla ya kufungwa rasmi kwa pazia la Ligi Kuu NBC Mei 30, mwaka huu.
