Na mwandishi wetu
Kocha wa zamani wa Yanga, Mwinyi Zahera amesema huu ni wakati sahihi wa mshambuliaji wa Clement Mzize kuihama Yanga na kutafuta changamoto kwingine ili kuimarisha kipaji na uwezo alionao.
Zahera ameeleza hayo leo Alhamisi wakati kukiwa na fununu za mchezaji huyo ambaye makabrasha yake yanaonesha ana miaka 20, kuwaniwa na baadhi ya timu vigogo ikiwemo Azam FC na Watford inayoshiriki Ligi ya Championship nchini England.
Zahera ambaye kwa sasa anainoa Namungo FC ameeleza: “Lazima (Mzize) aende nje ya nchi, maana hapa hawezi kuwa na muendelezo mazuri na kufanya zaidi ya sasa, sababu anazijua timu zote.
Zahera alifafanua kuwa anafahamu jinsi wanavyojifunza lakini kwa maendeleo yake lazima aende nje apate utofauti namna ya kucheza, ufundishwaji wake pia hata mbinu ni tofauti sana.
“Kwa nafasi yake anapaswa kusaidia timu kwenda mbali kama ilivyokuwa kwa Mayele (Fiston) ambaye alikuwa namba moja kwa ushambuliaji na asilimia 90 timu ilitegemea mabao yake na yeye sasa anapaswa kuwa hivyo kwa timu nyingine maana ameshakaa Yanga na bado hana uhakika wa nafasi lakini anafanya vizuri kulingana na umri wake,” alisema Zahera.
Mzize ambaye kwenye ushindi wa mwisho wa Yanga wa mabao 3-0 dhidi ya Singida FG alitoa asisti mbili, Zahera anaamini huu ni wakati wake wa kuwa mshambuliaji kiongozi wa timu kubwa.
Alisema kwamba jambo hilo litawezekana endapo Mzize atakubali kutafuta changamoto nyingine katika mataifa mengine yaliyoendelea zaidi kimiundombinu ya soka.
Mzize anayepata upinzani wa namba kutoka kwa Joseph Guede na Kennedy Musonda, licha ya kutofunga mabao mengi msimu huu lakini mpaka sasa ametoa pasi tano za mabao akizidiwa pasi tatu na kinara Kipre Junior wa Azam mwenye asisti nane.
Katika kikosi ch Yanga, Mzize anazidiwa na Stephane Aziz Ki na Kouassi Yao ambao kila mmoja ana asisti saba.
