Berlin, Ujerumani
Kiungo wa zamani wa Man United, Bastian Schweinsteiger amesema kwamba aliyekuwa kocha wa timu hiyo, Jose Mourinho alimpiga marufuku kufanya mazoezi na kikosi cha kwanza.
Schweinsteiger, mchezaji wa kimataifa wa Ujerumani, alicheza mechi nne tu Man United chini ya Mourinho na msimu uliofuata alijiunga na Chicago Fire ya Marekani ingawa msimu wa 2015-16, Luis Van Gaal akiwa kocha, mchezaji huyo alicheza mechi 31.
“Ilinihuzunisha sana kwa sababu United ilikuwa klabu ya pili niliyoipenda moyoni, nilijitoa kwa kiasi kikubwa wakati nikicheza pale, kwa hiyo ndiyo maana nilihuzunika,” alisema Schweinsteiger.
Schweinsteiger hata hivyo alisema pamoja na kukutana na madhila hayo lakini hakuwa mtu mwenye tabia ya kukimbilia kwenye vyombo vya habari badala yake kwake ilikuwa muhimu kufikiria soka na kuendelea na mwenendo wake kama awali.
Akikumbuka siku aliyopigwa marufuku kufanya mazoezi kikosi cha kwanza, Schweinsteiger alisema kwamba alipowasili Man United kwanza alifanya mazoezi na Zlatan Ibrahimovic na kuona ni jambo zuri kwa sababu ni mchezaji mwenye maono na ilikuwa jambo la kipekee kucheza pamoja naye.
“Siku iliyofuata ambayo ilikuwa siku yangu ya kuzaliwa nilikwenda Carrington (kwenye uwanja wa mazoezi), John Murtough alikuwa pale na kuniambia siruhusiwi kuingia kwenye vyumba vya kubadilishia nguo, kocha amesema hivyo.
“Nililazimika kumwambia anipe vifaa vyangu vya mazoezi, nikamuuliza sasa nitakuwa nafanya mazoezi na nani, naye akaniambia kuna timu ya vijana chini ya miaka 16, kwa hiyo nilikwenda na kufanya mazoezi na timu ya miaka 16,” alisema Schweinsteiger.
Schweinsteiger alisema kwamba siku pekee ambayo Mourinho alimuomba radhi ni baada ya kumwambia kwamba anaondoka Man United.
“Nilimuuliza Jose kama naweza kuondoka na hapo akaniomba radhi kwa kile alichonifanyia katika siku za mwanzo, na alilazimika kuniacha niondoke kwa sababu hangeweza tena kufanya lolote dhidi yangu,” alisema Schweinsteiger.
