Na mwandishi wetu
Kocha wa Mtibwa Sugar, Zuberi Katwila amekiri kuwa kufungwa bao 1-0 na KMC kumewaumiza na matokeo hayo yanaweza kuwagharimu kutokana na kuzikosa pointi tatu muhimu katika mchezo huo uliopigwa jana Jumanne kwenye Uwanja wa Manungu, Morogoro.
Katwila alisema kulingana na ratiba waliyonayo katika mechi nane zilizosalia, iliwapasa washinde mchezo huo lakini sasa imewaharibia mipango yao.
Kocha huyo hata hivyo alisema kwamba wanarudi uwanja wa mazoezi kupambana kurekebisha makosa na kuhakikisha saikolojia za wachezaji wao zinakaa sawa kuelekea mechi zinazofuata.
Katwila ambaye ni kocha wa zamani wa Ihefu FC alieleza kutoridhishwa na namna wanavyopoteza nafasi za kufunga mabao hata walipopata penalti na kushindwa kutumia nafasi hiyo kupindua matokeo.
“Kikubwa tumeshindwa kutumia nafasi tulizozipata, unaona mpaka penalti tumepoteza pia kwa hiyo ni vitu ambavyo vinatuumiza na pengine vitatugharimu zaidi kwa sababu huu ni mchezo muhimu na tumeupoteza tukiwa nyumbani, tungeshinda tungeanza kurejea sehemu salama,” alisema Katwila.
Mtibwa imeendelea kubaki mkiani baada ya mechi 22 ikiwa na pointi zake 17, ikiendelea pia kushikilia rekodi ya kufungwa mabao mengi zaidi, 37 mpaka sasa katika timu zinazoshiriki Ligi Kuu NBC msimu huu.
Soka Kocha Mtibwa aingiwa hofu
Kocha Mtibwa aingiwa hofu
Read also
