Na mwandishi wetu
Timu ya Simba imeelekea Zanzibar Jumanne hii kwa ajili ya kambi ya siku chache kujiandaa na mchezo wao dhidi ya Yanga utakaopigwa Jumamosi hii kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam.
Imeelezwa kuwa Simba inahitaji utulivu na kujiandaa vya kutosha kwa ajili ya mchezo huo ili kuhakikisha inaibuka na ushindi wa kwanza katika mechi hiyo ngumu baada ya kuukosa katika mechi nne zilizopita za michuano mbalimbali.
Wekundu hao waliibuka na ushindi mara ya mwisho Machi 15 wa mabao 2-0 dhidi ya Mashujaa katika mechi ya ligi kisha wakapoteza kwa jumla ya mabao 3-0 dhidi ya Al Ahly katika mechi mbili za robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika kabla ya kufungwa na Mashujaa kwa penalti 6-5 kwenye mech ya Kombe la FA na majuzi wakatoa sare ya 1-1 na Ihefu.
Meneja habari na mawasiliano Simba, Ahmed Ally alisema: “Kikosi kilirejea mazoezini Jumatatu na kimeelekea Zanzibar kwa ajili ya maandalizi ya mechi za ligi zinazokuja na kikosi kimeondoka na kipa Lakred (Ayoub) ambaye alikuwa nje kutokana na matatizo ya kifamilia.”
Upande wa Yanga yenyewe imeendelea kujipanga ikiwa Avic Town, Dar es Salaam kwa ajili ya mechi hiyo huku ikiwa na kumbukumbu ya ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Singida FG.
Kabla ya hapo Yanga ina kumbukumbu ya kutolewa kwa matuta 3-2 na Mamelodi Sundowns katika hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Soka Simba yaiendea Yanga Zanzibar
Simba yaiendea Yanga Zanzibar
Read also
