Na mwandishi wetu
Simba imeendelea kujiweka pagumu katika mkakati wa kulibeba taji la Ligi Kuu NBC baada ya kutoka sare ya bao 1-1 na Ihefu katika mechi iliyopigwa Jumamosi hii kwenye Uwanja wa Liti mjini Singida.
Katika mechi hiyo, Ihefu ndio waliokuwa wa kwanza kupata bao katika dakika ya 41 mfungaji akiwa ni Duke Abuya ambaye aliyatumia makosa ya kipa wa Simba Ally Salim kufunga bao hilo.
Simba walihaha kusawazisha bao hilo na juhudi zao kuzaa matunda dakika ya 71 kwa bao lililofungwa kwa penalti na Clatous Chama, penalti ambayo ilitolewa baada ya Kibu Dennis kuchezewa rafu.
Baada ya mechi hiyo kocha msaidizi wa Simba, Suleiman Matola aliwalaumu wachezaji wake kwa kukosa umakini wakati kocha wa Ihefu, Mecky Maxime aliwapongeza wachezaji wake kwa mchezo mzuri.
Simba ambayo hadi sasa imeshacheza mechi 20 za ligi hiyo inabaki katika nafasi ya tatu ikiwa na pointi 46 ikiwa imezidiwa na Azam FC inayoshika nafasi ya pili ikiwa na pointi 47 katika mechi 21.
Mahasimu wa Simba, Yanga ndio wanaoshika usukani wa ligi hiyo wakiwa na pointi 52 katika mechi 20 na Jumapili hii wanajitupa kwenye Uwanja wa CCM Kirumba mjini Mwanza kucheza mechi yao ya 21 ya ligi hiyo dhidi ya Singida Fountain Gate.
Soka Simba yajiweka pagumu ligi kuu
Simba yajiweka pagumu ligi kuu
Read also
