Johannesburg, Afrika Kusini
Polisi nchini Afrika Kusini wamearifu kuwa beki wa klabu ya Kaizer Chiefs ya nchini humo, Luke Fleurs (pichani) ameuawa kwa kupigwa risasi katika tukio lililohusisha wizi wa gari.
Kwa mujibu wa polisi mauaji hayo yalitokea usiku wa Jumatano kwenye kituo cha kuwekea mafuta jijini Johannesbrg katika kitongoji cha Florida.
Taarifa zilifafanua kuwa Fleurs mwenye umri wa miaka 24, alikuwa akisubiri kuwekewa mafuta ndipo watu wasiojulikana wakiwa na silaha walipomfuata na kumtaka atoke nje ya gari na mmoja wa watu hao kuondoka na gari hilo.
“Wauaji hao walimuoneshea silaha na kumtoa nje ya gari kabla ya kumpiga risasi,” alisema msemaji wa polisi katika mkutano wake na waandishi wa habari.
Uongozi wa Kaizer Chiefs, moja ya klabu kubwa nchini Afrika Kusini yenye mataji 12 ya ligi, ulisema kwamba kifo cha mchezaji huyo ni pigo kubwa kwao.
Klabu hiyo ilieleza kuwa polisi wanalishughulikia suala hilo na taarifa zaidi zitaendelea kutolewa kuhusu tukio hilo na uchunguzi wake.
Waziri wa Michezo wa Afrika Kusini, Zizi Kodwa alisema kwamba amesikitishwa na tukio hilo la uhai wa mtu kukatizwa kutokana na matukio ya kihalifu ya kijinai.
Fleurs alijiunga na Kaizer Chiefs mwaka jana baada ya kutamba na klabu ya SuperSport United na pia amewahi kuichezea timu ya vijana chini ya miaka 23 ya Afrika Kusini kwenye Michezo ya Olimpiki ya Tokyo mwaka 2021.
Kimataifa Beki Kaizer Chiefs auawa, aporwa gari
Beki Kaizer Chiefs auawa, aporwa gari
Read also
