Paris, Ufaransa
Kocha wa PSG, Luis Enrique (pichani) amewalaumu waandishi wa habari kwa kumuuliza kila wakati swali kuhusu maamuzi anayoyafanya kwa Kylian Mbappe akidai kwamba swali hilo linamkera.
Katika siku za hivi karibuni waandishi wa habari wamekuwa wakihoji nafasi ya Mbappe na muda anaocheza katika kikosi cha kwanza cha timu hiyo ya jijini Paris.
Maswali hayo yamekuwa yakiibuka baada ya Enrique kuanza kumuweka benchi kwa baadhi ya mechi ambazo amekuwa ama akiingia kipindi cha pili au akitolewa kabla ya dakika 90 kwisha.
Jumapili PSG ilitoka na ushindi muhimu wa mabao 2-0 dhidi ya mahasimu wao, Marseille licha ya kucheza wakiwa 10 kwa takriban dakika 50 lakini mazingira yote hayo na matokeo mazuri havikutosha kuwa sababu ya swali kuhusu Mbappe kutoulizwa.
Enrique aliulizwa kuhusu hatua yake ya kumtoa Mbappe katika dakika ya 65 ya mchezo huo na nafasi yake kuingia Goncalo Ramos, swali ambalo kocha huyo hakulifurahia.
“Ni mziki huo huo wiki baada ya wiki, inanikera, mimi ni kocha na nafanya maamuzi kila siku, kila wiki, nitakuwa nikifanya hivyo hivyo hadi siku yangu ya mwisho hapa Paris, wakati wote huwa natafuta suluhisho bora kwa timu yangu, labda nakosea lakini nadhani niko sahihi,” alisema Enrique.
Enrique ameendelea kumtoa au kutomuanzisha Mbappe kikosi cha kwanza tangu mshambuliaji huyo atangaze hadharani kwamba ataihama klabu hiyo baada ya msimu huu huku mazungumzo baina yake na klabu ya Real Madrid yakidaiwa kuendelea.
Kocha huyo hata hivyo Jumamosi alinukuliwa akisema anaamini Mbappe atabaki na kuendelea kuichezea timu hiyo na hadi sasa amekuwa na mchango mzuri ikiwamo kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya ambapo timu hiyo ipo hatua ya robo fainali ikisubiri kuumana na Barcelona.
