Na mwandishi wetu
Ikicheza bila kiungo wake nyota Pacome Zouazou, Yanga imeanza na sare ya 0-0 mechi ya kwanza ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini.
Kwa matokeo ya mechi hiyo iliyopigwa Jumamosi hii usiku, Yanga itakuwa na kazi moja kwenye mechi ya marudiano hapo Aprili 5, ni ama ipate ushindi wowote au sare ya mabao ili iweze kusonga mbele hatua ya nusu fainali.
Ikitokea kwa timu hizo kutoka sare ya bila kufungana kama ilivyojitokeza katika mechi ya kwanza, mikwaju ya penalti itatumika kuamua timu ipi isonge mbele.
Uimara wa safu za ulinzi pamoja na makipa ulikuwa kikwazo kwa pande zote kutoka uwanjani na mabao kwani licha ya takwimu kuonesha Mamelodi kumiliki mchezo kwa kiasi kikubwa lakini timu zote zilifanya mashambulizi ya nguvu lakini ulinzi imara ulikuwa kikwazo
Makipa Ronwen Williams wa Mamelodi na Djigui Diarra wa Yanga kwa nyakati tofauti kila mmoja alidhihirisha uwezo wake wa kukokoa michomo iliyoelekezwa langoni huku wakipata nguvu ya ulinzi wa mabeki wao.
Yanga ndio walioanza kuwasumbua Mamelodi katika dakika ya 27 baada ya Clement Mzize kuambaa na mpira na kufumua shuti ambalo hata hivyo liliishia mikononi mwa Williams.
Muda mchache baadaye, Mamelodi walijibu mapigo kupitia kwa Teboho Mokoena ambaye hata hivyo shuti lake la mbali licha ya kuwatia hofu mashabiki wa Yanga lakini halikuweza kuipa Mamelodi bao.
Kipindi cha pili pia kilitawaliwa na mashambulizi ya mara kwa mara ambayo hayakuweza kubadili matokeo ya mchezo kwani hadi dakika 90 zinamalizika hakuna timu iliyoliona lango la mwenzake.
Akizungumza baada ya mechi hiyo kocha wa Yanga, Miguel Gamondi aliwasifu wachezaji wake kwa kucheza vizuri na kutengeneza nafasi ingawa hawakuweza kuzitumia kupata ushindi.
Kwa upande wake kocha wa Mamelodi, Rhulani Mokwena alikiri timu yake kukutana na upinzani mkali lakini alisema anaamini katika mechi ya marudiano wana nafasi ya kufanya vizuri na kufuzu hatua ya nusu fainali.
Soka Yanga, Mamelodi hakuna mbabe
Yanga, Mamelodi hakuna mbabe
Read also
