Na mwandishi wetu
Kocha wa zamani wa Yanga, Hans van der Pluijm ameitahadharisha Mamelodi Sundowns kuwa inakwenda kukutana na miongoni mwa timu bora Afrika kwa sasa itakapovaana na Yanga.
Yanga na Mamelodi zitaumana kesho Jumamosi kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam katika mechi ya kwanza ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Pluijm aliyewahi kuipa Yanga mataji mawili mfululizo ya ligi kuu msimu wa 2014-15 na 2015-16 huku akisifika kwa soka safi lililopewa jina la ‘Kampa, kampa tena’ alisema hapingi ubora wa Mamelodi na nafasi ya ushindi wanayopewa.
Kocha huyo hata hivyo alisema anaamini lolote linaweza kutokea katika mchezo huo utakaopigwa kuanzia saa 3.00 usiku.
“Mpira una matokeo ya ajabu, msimu uliopita hakuna aliyeipa nafasi Yanga hata ya kufika makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika, lakini wakacheza fainali na kuwashangaza wengi.
“Binafsi naamini kwenye mipango ya kocha Miguel Gamondi, analijua vizuri soka la Afrika lakini kizuri zaidi anaifahamu Mamelodi na utamaduni wake na ana baadhi ya watu kutoka Afrika Kusini kwenye benchi lake, hivyo naamini atafanya vizuri kwenye mchezo huu,” alisema Pluijm.
Pluijm aliwataka pia wachezaji wa Yanga kuwaheshimu Mamelodi kwa kucheza kwa tahadhari kubwa wakitambua ubora na uimara wa wapinzani wao na kutumia kila nafasi watakayoipata ili kuhakikisha wanaumaliza mchezo nyumbani kabla ya mechi ya marudiano Ijumaa ijayo kwenye Uwanja wa Loftus Versfeld mjini Pretoria, Afrika Kusini.
