Na mwandishi wetu
Nahodha Msaidizi wa Yanga, Dickson Job amesema maandalizi yao kuelekea mchezo wa keshokutwa Jumamosi dhidi ya Mamelodi Sundowns yamekamilika na wamejipanga kwa ajili ya kushinda mchezo huo.
Yanga itakuwa nyumbani Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam kuikabili Mamelodi katika mchezo wa mkondo wa kwanza wa hatua ya robo fainali wa Ligi ya Mabingwa Afrika.
Akizungumza leo Alhamisi akiwa kambini kwao Avic Town, Kigamboni mlinzi huyo alisema wanajua uzito wa mchezo huo na umuhimu wa ushindi lakini wamejipanga kucheza kwa nidhamu na kufuata kile walichoelekezwa na makocha wao ili kutimiza lengo lao.
“Tupo tayari kimwili na kiakili kuikabili Mamelodi najua utakuwa mchezo mgumu lakini na sisi tunahitaji kushinda ili kufika hatua za juu kwenye mashindano hayo, najua mchezo utakuwa mgumu lakini tumedhamiria kuionesha Afrika kwamba Yanga ni timu bora,” alisema Job.
Mlinzi huyo alisema anajua watu wengi hawaipi Yanga nafasi ya kufanya vizuri katika mchezo huo kutokana na mafanikio ya wapinzani wao, Mamelodi lakini wamepanga kutumia dhana hiyo kuishangaza Afrika kwa kupata ushindi mnono utakaowapeleka hatua inayofuata.
Alisema wamedhamiria kutowapa nafasi wapinzani wao kupata hata bao moja na kila mchezaji atakayepata nafasi amejiandaa kutimiza majukumu yake kwa asilimia zote.
