Na mwandishi wetu
Kaimu kocha mkuu wa Taifa Stars, Hemed Suleiman ‘Morocco’ amesema anaiona Tanzania ikifika mbali katika soka kutokana na jitihada zinazofanywa na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).
Kocha huyo alisema kitendo cha kushiriki mashindano mbalimbali ikiwemo kushiriki michuano ya FIFA Series 2024 ni jitihada za wazi ambazo zinaonesha soka la Tanzania linapiga hatua.
“Nimeridhishwa na jitihada zinazofanywa na TFF, chini ya Rais Wallace Karia, ukweli naiona mbali Tanzania, kitendo cha kucheza mechi nyingi za kirafiki na mataifa makubwa kama Bulgaria kunawapa wachezaji uzoefu na kufanya wasiwe wageni katika ulimwengu wa mpira,” alisema Morocco.
Kocha huyo alisema jitihada hizo kama zitaendelea anaamini Tanzania itaishangaza Afrika kwenye michuano ya Mataifa ya Afrika 2027 ambayo itafanyika Tanzania kwa kushirikiana na mataifa ya Kenya na Uganda.
Alisema kingine kinachomvutia ni namna TFF inavyopambana kuwatafuta wachezaji wenye asili ya Tanzania kuitumikia timu yao ya taifa.
Alisema jambo hilo litaongeza ushindani dhidi ya wachezaji wanaocheza soka ligi ya ndani kitu ambacho kitaifanya timu hiyo kuwa bora kama yalivyo baadhi ya mataifa ya Afrika.
Morocco pia amewaomba wadau mbalimbali kuunga mkono jitihada zinazofanywa na TFF, ili Tanzania iwe miongoni mwa taifa linaloogopewa na kuheshimiwa katika mchezo wa soka kwani uwezo wa kufanya hivyo upo.
Soka Morocco aiona Tanzania ikifika mbali
Morocco aiona Tanzania ikifika mbali
Read also
