New York, Marekani
Nahodha wa timu ya taifa ya Argentina, Lionel Messi amesema umri pekee hauwezi kuwa sababu ya yeye kustaafu soka badala yake atafanya hivyo siku atakayoona hawezi tena kuisaidia timu kupata mafanikio.
Messi, 36, ambaye aliiongoza Argentina kubeba Kombe la Dunia mwaka 2022 nchini Qatar, hadi sasa hajaonesha dalili yoyote ya lini atastaafu na mkataba wake na klabu anayoichezea sasa ya Inter Miami FC ya Marekani unafikia ukomo Desemba 2025.
“Najua wakati ambao nitakuwa sichezi vizuri, wakati ambao nitakuwa mimi mwenyewe sifurahii, wakati ambao sitokuwa mwenye kuwasaidia wachezaji wenzangu,” alisema Messi.
“Huwa napenda kujifanyia tathmini, najua wakati nikiwa vizuri na wakati nikiwa hovyo, wakati nacheza vizuri na wakati nacheza vibaya na nitakapoona ni wakati wa kuchukua uamuzi wa kustaafu nitafanya hivyo bila kufikiria umri, nikijiona niko vizuri wakati wote nitajaribu kuendelea kushindana kwa sababu ni kitu ninachokipenda na najua namna ya kukifanya,” alisema Messi.
Messi ambaye amejipatia mafanikio zaidi akiwa na klabu ya Barcelona kabla ya kuhamia PSG ana rekodi ya kubeba tuzo nane za Ballon d’Or na anatarajia kuiongoza Argentina kwenye fainali za Copa America baadaye mwaka huu.
Akimzungumzia Messi hivi karibuni, kocha wa Inter Miami, Gerardo ‘Tata’ Martino alisema bado ni yule yule mwenye shauku ya ushindi kama ambavyo ilikuwa wakati akiwa kocha wake katika klabu ya Barcelona.
Naye kocha wa Argentina, Lionel Scaloni akimzungumzia Messi ambaye kwa sasa ni majeruhi, alisema ni mchezaji pekee ambaye ana uhakika wa nafasi kwenye kikosi chake.
