Na mwandishi wetu
Kocha mkuu wa timu ya taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’, Hemed Suleiman ‘Morocco’ amesema amepata kitu kikubwa kutokana na ushiriki wao kwenye michuano maalumu ya Fifa Series iliyofanyika Azerbaijan.
Stars ilianza michuano hiyo kwa kufungwa bao 1-0 na Bulgaria kabla ya kusahihisha makosa yao na kupata ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Mongolia kwenye Uwanja wa Dalga, jana.
Mabao ya Stars kwenye mchezo huo yaliwekwa kimiani na mshambuliaji wa KRC Genk ya Ubeligiji, Kelvin John, Abdul Suleiman wa Azam na kiungo Novatus Dismas wa Shaktar Donetsk ya Ukraine.
“Tumejifunza mambo mengi kutokana na ushiriki wetu kwenye haya mashindano ambayo tutayatumia kwa ajili ya mashindano mengine tutakayoshiriki. Yamewajengea wachezaji wetu chipukizi uzoefu utakaowasaidia siku zijazo,” alisema Morocco.
Akiuzungumzia kiufundi mchezo wao dhidi ya Mongolia alisema wangeweza kupata mabao mengi zaidi ya waliyofunga kama washambuliaji wake wangetumia kila nafasi zilizotengenezwa.
“Tumeshinda mechi baada ya kupoteza mchezo wetu wa kwanza dhidi ya Bulgaria. Nawashukuru wachezaji wangu kwa kujitoa lakini bado tungeweza kufunga mabao mengi zaidi kama wangetumia nafasi zote tulizotengeneza,” alisema Morocco.
