Na mwandishi wetu
Simba leo Jumanne imevunja kambi ya siku saba Zanzibar na kurejea Dar es Salaam huku ikiwa na siri nzito kuelekea mchezo wao wa mkondo wa kwanza wa robo fainali wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Al Ahly.
Kuelekea mchezo huo utakaopigwa Ijumaa hii kwenye Uwanja wa Mkapa Dar es Salaam, kocha msaidizi wa Simba, Selemani Matola alisema kambi hiyo imewaimarisha kwa kiasi kikubwa na imewaongezea wachezaji ari ya kupambana kupata ushindi katika mechi hiyo wanayoipa uzito mkubwa.
“Tumerejea tukiwa na nguvu mpya, kitu kizuri ni kwamba tumefikia kambini kwa ajili ya kuongeza vitu viwili vitatu kwa wachezaji wetu ambao wameahidi kupambana kufa au kupona kwa ajili ya kuipa Simba ushindi kwenye ardhi ya nyumbani,” alisema Matola.
Alisema wanatambua mchezo huo utakuwa na ushindani mkubwa kutokana na wapinzani wao kukutana mara nyingi, lakini silaha kubwa wanayojivunia nayo kuelekea kwenye mchezo huo ni uwepo wa kocha mkuu Abdelhak Benchikha kwenye benchi lao.
Alisema kocha huyo anawajua vyema wapinzani wao ikiwemo mbinu zao ‘chafu’ zinazowapa ushindi hivyo katika maandalizi yao amewapa wachezaji silaha muhimu ambazo kama wachezaji wakizitumia ipasavyo anaamini watavuna ushindi mnono wakiwa nyumbani.
Matola amewaomba mashabiki wa timu hiyo kujitokeza kwa wingi uwanjani ili kuipa sapoti timu yao na kutengeneza rekodi ya pili kwa kumtoa bingwa mtetezi katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Simba inakumbukwa kwa kuweka rekodi mara ya mwisho mwaka 2003 kwa kuitoa Zamalek pia ya Misri na kuingia makundi na kuwa timu ya kwanza Tanzania kuitoa timu ya Misri katika michuano hiyo.
Soka Simba yavunja kambi Zanzibar
Simba yavunja kambi Zanzibar
Read also
