Barcelona, Hispania
Beki wa zamani wa timu ya taifa ya Brazil na klabu ya Barcelona, Dani Alves ametoka jela (lupango) baada ya kulipa dhamana ya Pauni 1.1 milioni aliyotakiwa kulipa wakati akisubiri uamuzi wa rufaa aliyokata kuhusu kesi ya kubaka inayomkabili.
Alves ambaye pia amewahi kuichezea PSG ya Ufaransa, mwezi uliopita, alihukumiwa kwenda jela miaka minne na nusu kwa kosa hilo analodaiwa kulifanya usiku mmoja wa Desemba 2022 katika klabu moja ya usiku mjini Barcelona.
Jumatano iliyopita alipewa dhamana lakini akalazimika kuendelea kubaki kifungoni baada ya kushindwa kupata fedha kwa ajili ya kulipa dhamana hiyo kama alivyotakiwa na mahakama.
Akiwa na wakili wake, Alves alionekana jana Jumatatu akitoka katika Gereza la Brians 2 lililopo Kaskazini Magharibi mwa jiji la Barcelona majira ya saa 10 za jioni.
Habari za ndani zinadai kwamba baada ya kutajiwa kiasi cha pesa ambacho angekitoa kwa ajili ya dhamana, mchezaji huyo alianza kuhaha kutafuta fedha hizo na hatimaye alifanikisha malipo hayo Ijumaa iliyopita na jana Jumatatu mahakama ilithibitisha kupokea malipo hayo na hivyo kumuachia kwa dhamana.
Awali ilitarajiwa familia ya mwanasoka mwingine wa Brazil, Neymar ingemlipia mchezaji huyo dhamana lakini baadaye baba mzazi wa Neymar alisema kwamba familia yake inajitoa katika suala hilo kwa kuwa mahakama imemkuta mchezaji huyo na hatia.
Masharti mengine ya dhamana aliyopewa Alves mbali na malipo ya fedha ni pamoja na kuwasilisha hati zake za kusafiria za Hispania na Brazil katika mamlaka husika za Hispania na kutomsogelea karibu kwa umbali usiozidi mita 1,000 msichana anayedaiwa kumbaka.
Alves ambaye ana mjengo wa kifahari mjini Barcelona pia amepigwa marufuku kutoka nje ya Hispania, masharti ambayo wakili wake ameahidi kuyapinga hasa suala zima la malipo ya fedha kwa hoja kwamba ni kama vile mtu asiye na pesa hana haki ya kupewa dhamana.
Kimataifa Dani Alves atoka lupango
Dani Alves atoka lupango
Read also
