London, England
Winga wa Arsenal, Bukayo Saka amejitoa katika kikosi cha timu ya taifa ya England kutokana na kuwa majeruhi na hivyo atazikosa mechi mbili za kirafiki za timu hiyo dhidi ya Brazil na Ubelgiji.
Kwa mujibu wa FA, Saka, 22, ameshindwa kufanya mazoezi na timu hiyo tangu ajiunge nayo kwa ajili ya mechi hizo na hivyo amerudi katika kikosi cha Arsenal kinachojinoa kwa ajili ya mechi kali dhidi ya Man City ambayo itapigwa Machi 31.
Kwa upande wa England itaanza kwa kuumana na Brazil mechi ambayo itapigwa Jumamosi ijayo kwenye dimba la Wembley na kufuatiwa na mechi dhidi ya Ubelgiji ambayo itapigwa Machi 26.
Hatua ya mchezaji huyo kujiondoa katika kikosi hicho bila shaka inakuwa pigo kwa kocha wa timu hiyo Gareth Southgate anayeiandaa timu hiyo kwa ajili ya fainali za Kombe la Ulaya 2024 au Euro 2024.
England baada ya mechi hizo itakuwa na mechi nyingine mbili za mwisho za kirafiki dhidi ya Bosnia-Herzegovina itakayopigwa Juni 3 na kufuatiwa na mechi nyingine dhidi ya Iceland itakayopigwa Juni 7.
Baada ya hapo timu hiyo itaelekea Ujerumani kwa ajili ya fainali hizo zitakazotimua vumbi kwa kipindi cha mwezi mmoja kuanzia Juni 11 mwaka huu.
Kimataifa Saka ajitoa kwenye kikosi cha England
Saka ajitoa kwenye kikosi cha England
Read also