Na mwandishi wetu
Kocha mkuu wa Yanga, Miguel Gamondi amewapongeza wachezaji wake kwa kuendelea kupata ushindi katika mechi za Ligi Kuu NBC licha ya uchovu unaotokana na ratiba ngumu.
Yanga jana Alhamisi iliifunga Geita FC bao 1-0, ushindi ambao umeendelea kuwaweka kileleni mwa msimamo wa ligi wakifikisha pointi 52 huku wakiwa na mchezo mmoja mkononi dhidi ya timu inayoshika nafasi ya pili, Azam FC.
“Pamoja na ushindi lakini hatukuwa bora kama inavyokuwa mechi zilizopita, tumekuwa tukicheza mechi kila baada ya siku mbili huu ni utaratibu wa ajabu, nilijua mchezo ungekuwa mgumu lakini nafurahi kuona licha ya uchovu walionao vijana wangu, tumepata pointi tatu hicho ndio kilikuwa cha muhimu,” alisema.
Kocha huyo alisema kutokana na kukabiliwa na mchezo mgumu dhidi ya Azam FC keshokutwa Jumapili, hawatofanya maandalizi yoyote ili wachezaji wake waitumie mechi dhidi ya Geita kama mazoezi na kupata muda mzuri wa kupumzika kwa ajili ya mchezo huo.
Naye kocha mkuu wa Geita FC, Denis Kitambi alisema kilichosababisha wapoteze mchezo huo ni wachezaji wake kucheza kwa kujihami wakiwahofia wapinzani wao Yanga.
Alisema kwa kufanya hivyo waliwaruhusu kuwashambulia, kitu ambacho ilikuwa ni kujiweka kwenye uhatari wa kuruhusu bao tofauti na kama wangekuwa wanajibu mapigo kwenda kwenye lango lao.
“Hatukuwa kwenye ubora wetu, tuliwakaribisha kwenye lango letu wakafanya wanavyotaka, kitu ambacho kilikuwa ni hatari kwetu, angalau kipindi cha pili tulijaribu kutoka kwenda kuwashambulia lakini muda ulishakwenda,” alisema Kitambi.
Soka Gamondi alalamikia ratiba ngumu
Gamondi alalamikia ratiba ngumu
Read also
