Na mwandishi wetu
Kocha msaidizi wa Simba, Selemani Matola amesema licha ya ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Singida Fountain Gate kwenye Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam, hajafurahishwa na safu yake ya ulinzi.
Matola alisema kwamba hakufurahishwa na safu hiyo kutokana na kuruhusu mabao katika michezo mitatu mfululizo iliyopita.
Ushindi huo umeifanya Simba kufikisha pointi 42 na kuendelea kusalia nafasi ya tatu kwenye msimamo wa Ligi Kuu NBC huku Singida FG wakiendelea kuporomoka na kushika nafasi ya 12 wakiwa na pointi 21.
“Baada ya kupata mabao matatu kipindi cha kwanza wachezaji waliridhika na kutaka kucheza kwa kujiachia, tukawapigia sana kelele warudi mchezoni maana walileta matatizo na kuruhusu bao moja.
“Kama tungekuwa makini tungepata mabao zaidi ya haya, niwapongeze wachezaji wangu na mashabiki waliokuja kutupa sapoti kwani pointi tatu zilikuwa muhimu kwetu,” alisema Matola.
Alisema kitendo cha kuruhusu mabao matatu kwenye mechi tatu mfululizo si ishara nzuri na anaamini ni wakati wa kurudi kwenye uwanja wa mazoezi kurekebisha hilo ili wasiruhusu mabao kama hayo katika michezo inayofuata.
Kocha msaidizi wa Singida FG, Ngawina Ngawina alisema ni matokeo ya kusikitisha lakini anawapongeza Simba kwa kupata ushindi na kipindi cha kwanza walitengeneza nafasi nyingi na kimchezo walikuwa na uwezo mkubwa wa kupata mabao mengine zaidi.
“Tulipoenda mapumziko tukaongea na vijana, walifanya kazi walijitahidi kupambana lakini bado Simba walikuwa imara, tumekubali matokeo tunaenda kurekebisha makosa,” alisema Ngawina.
