Na mwandishi wetu
Mabondia Hassan Mwakinyo (pichani juu) na Abdallah Pazi ‘Dulla Mbabe’, kila mmoja ameweka bayana kuwa yuko jikoni akijiandaa na jambo kubwa.
Mwakinyo aliyeshinda pambano la hivi karibuni dhidi ya bondia kutoka Ghana, Elvis Ahorgah lililofanyika Zanzibar alisema anajiandaa na pambano kubwa Aprili, mwaka huu.
“Kuna kitu tunapika, nina hamu ya kuonesha,” aliandika ujumbe huo kwenye mtandao wake wa kijamii wa Instagram.
Hata hivyo, kwa mujibu wa mtandao wa ngumi wa kimataifa wa boxrec, Mwakinyo anatarajia kupanda ulingoni Aprili 27, mwaka huu kuchuana na Rasheed Adeyamo kutoka Nigeria kuwania mkanda wa WBO Afrika.
Kwa upande wake Dulla Mbabe (pichani chini) ameiambia GreenSports: “Ninajipanga, kuna jambo kubwa nitatangaza Machi 31, niwaambie mashabiki zangu wakae mkao wa kula, kwani kimya kingi kina mshindo mbele.”

Mara ya mwisho, Dulla Mbabe alimchapa bondia kutoka Malawi, Limbani Lano kwenye pambano lililopigwa mkoani Tanga, Januari, mwaka huu ikiwa ni wiki chache tangu alipotoka kupoteza dhidi ya Erick Katompa wa DR Congo, Novemba, mwaka jana.
