Accra, Ghana
Timu ya taifa ya soka ya wanawake ya Tanzania chini ya miaka 20, Tanzanite Queens, leo Jumanne inatupa karata yake ya pili dhidi ya Ghana katika mechi za Kundi A kwenye michuano ya 13 ya Afrika inayoendelea nchini humo.
Katika mchezo wa kwanza uliochezwa kwenye Uwanja wa Cope Coast, Tanzania ilitoka sare ya bao 1-1 dhidi ya majirani zao, Uganda.
Kuelekea mchezo huo kocha mkuu wa Tanzanite, Bakari Shime alisema maandalizi yao yamekamilika kwa asilimia 100 na anaamini wachezaji wake watacheza kwenye kiwango bora tofauti na ilivyokuwa kwenye mechi ya kwanza dhidi ya Uganda.
“Hatukuwa na muda mzuri wa kujiandaa baada ya mchezo wa kwanza lakini tumefanyia kazi mapungufu yetu na baada ya kuzoea hali ya hewa naamini tutacheza vizuri na kupata ushindi utakaotuweka katika mazingira mazuri ya kutinga hatua ya nusu fainali,” alisema Shime.
Kocha huyo alisema pamoja na kutowajua vizuri wapinzani wao Ghana, anaamini mchezo utakuwa mgumu na wenye ushindani lakini anajivunia ubora wa wachezaji alionao kwenye kikosi chake kwamba watampa matokeo mazuri.
Naye kocha mkuu wa Ghana ‘Black Princesses’, Yusuf Basigi alisema wanataka kushinda mchezo huo ili kujikita kileleni mwa kundi hilo na kuweka matumaini ya kucheza hatua inayofuata ya nusu fainali.
“Ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Ethiopia umetupa nguvu ya kutimiza malengo yetu kwenye michuano hii, najua Tanzania ni miongoni mwa mataifa yanayokuja kwa kasi kwenye mpira wa wanawake Afrika lakini tumejipanga kushinda ukizingatia tutakuwa mbele ya mashabiki zetu,” alisema Basigi.
Soka Tanzanite vitani dhidi ya Ghana
Tanzanite vitani dhidi ya Ghana
Read also
