Na mwandishi wetu
Yanga imeendelea kudhihirisha ubabe wake kwenye Ligi Kuu NBC baada ya kuichapa Ihefu FC mabao 5-0 katika mechi iliyopigwa Jumatatu hii kwenye Uwanja Azam Complex, Dar es Salaam.
Kipigo hicho kimezima matumaini ya baadhi ya mashabiki waliodhani Ihefu ingeweza kuizuia kasi ya Yanga baada ya kuichapa mabao 2-1 katika mzunguko wa kwanza na safari hii imeonekana kuwa imara ikiongezewa nguvu na baadhi ya wachezaji waliokuwa Singida Fountain Gate.
Mambo hata hivyo yaligeuka kuwa kinyume na matarajio hayo, badala yake Ihefu ikajikuta ikipigwa mkono, kipigo ambacho pia Yanga imempa hasimu wake Simba katika mechi ya ligi mzunguko wa kwanza.
Yanga ilipata mabao yake mawili kabla ya timu hizo kwenda mapumziko yakifungwa na Pacome Zouazoua na Mudathir Yahya, wote wakitumia vizuri pasi kutoka kwa Stephanie Aziz Ki.
Aziz Ki baada ya kupika mabao hayo mawili aliifungia timu yake bao la tatu ambalo ni la 12 kwake kwenye ligi hiyo hivyo kufungana na Feisal Salum ‘Fei Toto’ wa Azam FC ambaye pia amefunga mabao 12 hadi sasa.
Nyota ya Augustine Okrah nayo iling’ara katika mechi hiyo baada ya kuifungia timu yake bao la nne na kwa mara nyingine juhudi za Aziz Ki zilionekana alipotoa pasi iliyozaa bao hilo.
Karamu ya mabao ya Yanga ilihitimishwa na Maxi Nzengeli kwa kufunga bao la tano na la mwisho na kuifanya Yanga iongeze idadi ya timu ilizozifunga mabao matano ambapo mbali na Simba na Ihefu, timu nyingine zilizokutana na kipigo hicho nchini ni JKT Tanzania na KMC.
Ushindi huo unaifanya Yanga kuendelea kujiimarisha kileleni mwa msimamo wa ligi kwa kufikisha pointi 49 katika michezo 18 huku ikiwa imetupia kambani mabao 47.
Soka Yanga yaipiga Ihefu mkono
Yanga yaipiga Ihefu mkono
Read also
