Na mwandishi wetu
Beki wa zamani wa Simba, Azam FC na Singida Fountain Gate, Pascal Wawa amesema kuwa baada ya kuutumikia mpira kama mchezaji sasa ni wakati wa kuanza safari ya ukocha ili kuibua vipaji vipya.
Wawa aliyasema hayo leo Jumatatu akiwa kwenye kozi ya ukocha ya Grassroots ambayo inashirikisha washiriki 42 chini ya uratibu wa Chama cha Mpira wa Miguu Wilaya ya Ilala (IDFA).
“Baada ya kumaliza muda wangu wa kucheza kama mchezaji sasa ni wakati wa kuingia kwenye hatua nyingine ya maisha yangu kwenye soka kwa kwenda kuibua vipaji vipya kama walivyonishika mkono mimi wakati naanza safari yangu.
“Kusoma kozi ya ukocha hii ilikuwa ndoto yangu ya muda mrefu siku moja nije kuwa kocha, naamini inaenda kutimia kwa sababu safari yangu ndio kwanza imeanza na haitaishia hapa,” alisema Wawa.
Wawa alisema kuwa ana uzoefu wa kutosha kwenye soka kwa kupita mataifa makubwa kisoka kama kwao Ivory Coast, Tanzania na Sudan na atatumia mafunzo hayo kwa ajili ya kuendeleza alichonacho kwenye ukocha.
