Na mwandishi wetu
Simba na Yanga kesho Jumanne zitawafahamu wapinzani wao kwenye hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika katika droo itakayochezeshwa jijini Cairo, Misri kuanzia saa 1.00 jioni kwa saa za Afrika Mashariki.
Timu nyingine ambazo ziko kwenye droo hiyo ni Al Ahly (Misri), ASEC Mimosas (Ivory Coast), Mamelodi Sundowns (Afrika Kusini), Atletico Petroleos (Angola), TP Mazembe (DR Congo), na Esperance Sportive de Tunis ya Tunisia.
Michezo ya awali ya hatua ya robo fainali inatarajiwa kupigwa kati ya Machi 29 na 30 huku michezo ya marejeano ikitarajiwa kuchezwa kati ya Aprili 5 na 6, mwaka huu.
Kulingana na kanuni, Yanga na Simba ambao wote wamemaliza wa pili katika makundi yao, mmoja wao anaweza kukutana na Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini kwa mara ya kwanza katika historia yao.
Mamelodi Sundowns tangu ianzishwe mwaka 1970, haijawahi kukipiga na Yanga na Simba hivyo kuufanya mchezo huo kusubiriwa kwa hamu na wapenzi wengi wa mpira wa miguu hapa nchini.
Sundowns wametawala soka la Afrika Kusini kwa kushinda taji hilo kwa misimu mitano mfululizo 2018/2019, 2019/2020, 2020/2021, 2021/2022 na 2022/2023 na kwa sasa ndio vinara wa Ligi Kuu Afrika Kusini wakiwa na pointi 42 baada ya mechi 16.
Petro de Luanda kutoka Angola pia inaweza kuwa wapinzani wa Yanga au Simba kulingana na droo ya CAF, ni miongoni mwa timu bora katika robo fainali ya Ligi ya Mabingwa baada ya kumaliza hatua ya makundi wakiwa na rekodi nzuri ya pointi 12 bila kupoteza mchezo wowote.
Kuhusu Al Ahly, Simba imekutana mara nne kwenye Ligi ya Mabingwa miaka ya karibuni na mara mbili katika Afrika Football League (AFL).
Simba imeshinda mara mbili, Al Ahly wameshinda mbili na kutoka sare mara moja. Kwenye AFL, Al Ahly walitoka sare ya 2-2 kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam na mchezo wa marudiano ulimalizika kwa sare nyingine ya 1-1 Oktoba, mwaka jana.
Yanga na Asec Mimosas pia wanaweza kukutana baada ya kuwa wameshakutana mara mbili kwenye historia, Yanga wakipoteza 3-0 nyumbani na baadaye 2-1 ugenini kwenye hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa mwaka 1998.
Asec Mimosas ni moja ya timu bora kwenye mashindano hayo ikiwa na uzoefu mkubwa kwenye Ligi ya Mabingwa. Wamemaliza nafasi ya kwanza Kundi B wakiwa na pointi 11, pia wameshinda taji la Ligi Kuu Ivory Coast mara 29 na taji la Ligi ya Mabingwa mwaka 1998.
Kimataifa Simba, Yanga nani kupewa Mamelodi Ligi ya Mabingwa Afrika?
Simba, Yanga nani kupewa Mamelodi Ligi ya Mabingwa Afrika?
Read also
