Dakar Senegal
Wakati hatma ya Sadio Mane ikiwapasua vichwa mashabiki wa Liverpool, mchezaji huyo ameibuka na kauli inayoonekana kama kuwatoa hofu mashabiki hao.
Akizungumza baada ya kutupia mara tatu wakati Senegal ikiilaza, Benin mabao 3-1 jana katika mechi ya kuwania kufuzu Afcon 2023, Mane alisema anawaheshimu mno mashabiki wa Liverpool na hata kauli yake kwamba mashabiki wa Senegal ndio wanaoamua hatma yake ilikuwa ni ya utani.
Hatma ya mchezaji huyo katika klabu ya Liverpool imekuwa haieleweki katika wiki za hivi karibuni iwapo atabaki au ataondoka na aliwahi kusema kwamba baada ya mechi ya fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Real Madrid angesema anaelekea wapi.
Hadi sasa hajasema wapi anataka kuelekea hasa baada ya Liverpool kulala kwa bao 1-0 mbele ya Real Madrid katika mechi hiyo iliyopigwa Mei 28 lakini inaaminiwa na wengi kwamba mchezaji huyo anataka changamoto mpya. sehemu nyingine.
Habari hiyo inabebwa na ukweli kwamba Mane amekuwa akitakiwa na klabu kadhaa za Ulaya mojawapo inayotajwa zaidi ni Bayern Munich ya Ujerumani ambayo inadaiwa kufuatilia kwa karibu nyenendo za mchezaji huyo na suala zima la uhamisho.
Mane aliibua sintofahamu kwenye mitandao ya kijamii baada ya kutoa kauli kwenye mkutano na waandishi wa habari kabla ya mechi ya Senegal na Benin jana alipogusia mpango wake wa kutaka kuondoka Livepool lakini aliwashangaza watu pale alipowahusisha watu wa Senegal na mpango huo.
“Je si ni kweli kwamba kati ya asilimia 60 hadi 70 ya watu wa Senegal wanataka mimi niondoke Liverpool, nitafanya wanachokitaka, tutaona hivi karibuni, yajayo yatazungumza.
Akizungumza baada ya mechi hiyo ya Senegal, Mane hata hivyo alifafanua kuwa alichokisema ilikuwa ni utani. “Nilichozungumza jana nilikuwa katika hali ya utani, ni dhihaka kidogo na imekwenda kila mahali, nafikiri tuishie hapo.”
“Liverpool ni klabu ninayoiheshimu sana, mashabiki wamenikubali tangu siku ya kwanza, kuhusu mambo yangu ya baadaye tutaona itakavyokuwa.”
Liverpool tayari imetangaza kwamba haitokuwa tayari kumuuza Mane kwa ada chini ya Pauni 40 milioni na kocha Jurgen Klopp ametaka kuwapo na mbadala wa mchezaji huyo kabla uamuzi wa kumuuza haujafikiwa. Mane ana mwaka mmoja katika mkataba wake Liverpool.
Kimataifa Mane awatoa hofu mashabiki Liverpool
Mane awatoa hofu mashabiki Liverpool
Related posts
Read also