Riyadh, Saudi Arabia
Bondia Anthony Joshua amemchakaza kwa KO ya raundi ya pili mpinzani wake, Francis Ngannou katika pambano la ngumi za uzito wa juu lililofanyika usiku wa jana Ijumaa mjini Riyadh.
Ngannou alikumbana na kipigo hicho kwa ngumi ya mkono wa kushoto iliyomkuta chini ya kidevu kabla ya kuanguka chini na kujikuta akipoteza fahamu.
Baada ya kuanza kuhesabiwa na kukaa sawa, Ngannou, mwenye umri wa miaka 37 ilidhihirika wazi kwamba asingeweza kuendelea na pambano hilo hasa baada ya watu wa huduma ya kwanza kuanza kumpa msaada.
Katika pambano hilo, Joshua alianza kuonesha makali yake raundi ya kwanza baada ya kumchapa Ngannou ngumi kali ya mkono wa kulia ambayo ilimyumbisha lakini aliweza kusimama imara na kuendelea na pambano.
Johua, 34 katika raundi ya pili aliendeleza makali yake kwa kumchapa Ngannou ngumi nyingine ambayo ilimpiga kisawasawa kwenye sehemu ya sikio la upande wa kushoto.

Ngumi hiyo kali hata hivyo haikumtetemesha sana Ngannou ambaye alionekana kuwa imara na kuendelea na pambano lakini alikutana na ngumi nyingine kali ya mkono wa kulia iliyotosha kumfanya alambe sakafu na kushinda kuendelea na pambano.
Unapoelekea kwenye kuutafuta ubingwa wakati wote unatakiwa kuwa makini, huyu ni mimi ambaye nilijitoa kwa ajili ya mpango huo,” alisema Joshua baada ya ushindi huo.
“Nilipomuona Ngannou kwenye pambano na Tyson Fury nilijisemea, kumbe huyu jamaa anaweza kupigana, nahitaji ‘kitu cha aina hii’,” alisema Joshua.
Baada ya kipigo hicho, Ngannou aliibukia kwenye mitandao ya kijamii akitumia akaunti yake ya Twitter au X kuwaomba radhi mashabiki wake kwa madai kwamba amewaangusha lakini akawataka wasikate tamaa.
“Samahani jamani, nimewaangusha, leo ilikuwa siku mbaya kwenye ofisi yangu lakini kesho itakuwa siku nyingine, asanteni kwa mapenzi yenu,” alisema Ngannou.
