Na mwandishi wetu
Ili kuhakikisha inamaliza migogoro kwenye sekta ya michezo, Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo imeunda mahakama ya usuluhishi na kuja na katiba ya mfano itakayofuatwa na vyama na mashirikisho yote nchini.
Hayo yameelezwa Jumatano hii jiini Dar es Salaam na Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Damas Ndumbaro katika mkutano na viongozi wa vyama na mashirikisho ya michezo kujadili maendeleo ya michezo nchini.
“Ili kuhakikisha migogoro inakufa tunakuja na katiba ya mfano ambayo itafuatwa na vyama vyote na tumeunda kamati ya watu 11 ambao wataisimamia na kushauri serikali ambayo inaongozwa na Leonard Thadeo,” alisema Ndumbaro.
Pia alisema wameunda Kamati ya mahusiano kati ya vyama na serikali ambayo itakuwa na wajumbe nane na mwenyekiti wake ni Dk Yusuf Singo.
Ndumbaro pia aliwataka viongozi wa vyama kuwa wazi katika fedha wanazopokea kwa kuzitolea taarifa ni nani kawapa kwa sababu duniani kuna tatizo la utakatishaji fedha na Tanzania ni moja ya nchi inayotajwa katika tuhuma hizo.
“Hatukupangii kiasi cha kutumia ila ukipata fedha utawajibika kutoa taarifa nani kakupa na lazima vyama muwe na ofisi na vyama vitakavyobainika kutokuwa na ofisi tutavifungia,” alisema Ndumbaro.
Dk Ndumbaro alihitimisha kwa kufafanua kuwa kamati zilizoundwa zitakutana Dodoma Juni, mwaka huu ili kutoa taarifa ya majukumu waliyopewa kutekeleza.
