Miami, Marekani
Kocha mkuu wa timu ya taifa ya England, Thomas Tuchel ametetea maamuzi yake katika mechi ya nusu fainali ya Kombe la Dunia 2026 dhidi ya Argentina licha ya timu hiyo kushindwa.
Akizungumza kabla ya mechi ya kusaka mshindi wa tatu dhidi ya Ufaransa, kocha huyo Mjerumani alisema kama anahitajika mtu wa kulaumiwa basi yeye yuko tayari kubeba zigo la lawama.
Tuchel hata hivyo alisema hana cha kujutia na kuongeza kuwa timu yake ndiyo iliyoumizwa zaidi kuliko yeyote na kwamba kilichotokea ni jeraha ambalo wanalazimika kulibeba.
Katika mechi hiyo, England walikuwa wakipambana kuweka rekodi ya kufikia hatua ya fainali ya Kombe la Dunia mara ya kwanza tangu kufanya hivyo mara ya mwisho mwaka 1966, miaka 60 iliyopita.
Kilichotokea katika mechi hiyo kiliiumiza mno England kwani baada ya kuongoza kwa bao 1-0 mambo yalibadilika mwishoni na kujikuta wakilala kwa mabao 2-1 huku wakipigwa presha na Messi.
Mabao ya Argentina yaliyopatikana dakika za 85 na 90 (+2) yaliwaumiza mno mashabiki wa England huku baadhi ya wachambuzi wakilaumu maamuzi kadhaa ya Tuchel ikiwamo kujihami zaidi badala ya kushambulia.
Alipoulizwa ni kwa nini timu yake ilicheza kwa kujihami zaidi Tuchel alisema hicho ndicho kilichotakiwa kufanywa kwa namna Argentina walivyokuwa na hajutii uamuzi wake katika hilo.
“Nilichukua maamuzi mengi, niliamini fikra zangu, uzoefu wangu, niliamini katika upambanaji wangu na nilichukua maamuzi kwa lengo la kuisaidia timu kupata matokeo lakini hatukupata matokeo,” alisema Tuchel.
England inacheza mechi ya kusaka mshindi wa tatu dhidi ya Ufaransa, mechi itakayopigwa Jumamosi Julai 18, 2026 wakati mechi ya fainali kati ya Argentina na Hispania itapigwa Jumapili Julai 19, 2026.
