Arlington, Texas
Nahodha na mshambuliaji wa timu ya taifa ya Ufaransa, Kylian Mbappe inaonekana hajakubaliana na mbinu za kocha wa timu hiyo, Didier Deschamps katika mechi yao ya nusu fainali ya Kombe la Dunia 2026 dhidi ya Hispania.
Ufaransa iliumana na Hispania Jumanne Julai 14, 2026 na kulala kwa mabao 2-0 na hivyo kuinyima timu hiyo rekodi ya kufuzu hatua ya fainali ya Kombe la Dunia kwa mara ya tatu mfululizo.
Mbappe ameifungia Ufaransa mabao manane katika fainali hizo na sasa anasubiri mechi ya kusaka mshindi wa tatu itakayopigwa Jumamosi Julai 18, 2026 dhidi ya England au Argentina.
Idadi hiyo ya mabao ya Mbappe ni sawa na yale aliyofunga miaka minne iliyopita katika fainali za Kombe la Dunia za Qatar 2022 ambapo timu hiyo ilifikia hatua ya fainali na kupoteza kwa mikwaju ya penalti mbele ya Argentina.
Akifafanua zaidi kuhusu mechi yao na Hispania ilivyokuwa Mbappe alisema kwamba timu ilzidiwa na kutaja eneo la kiungo ambalo alisema Hispania walionekana kuwa wengi.
“Katika mechi na Hispania katikati ilikuwa watatu dhidi ya wawili, hapo kuna ugumu na Fabian (Ruiz) na Rodri walikuwa na fursa ya kujidai, nafikiri ilipaswa kuwa mtu na mtu, kuwalazimisha wakimbizane na sisi,” alisema Mbappe.
Mbappe alisema Ufaransa hawakucheza mchezo walioutaka kimbinu na kiufundi na ndio maana walishindwa kwa sababu hawakufanya kilichotakiwa kufanywa katika mechi ya nusu fainali ya Kombe la Dunia.
Kwa upande mwingine alisema Hispania waliheshimu aina yao ya uchezaji na kile wanachokifanya siku zote yaani kupenda kumiliki mipira na kuwa na kasi na mbinu ya Ufaransa ilitakiwa ya kuwabana ili wasiwe katika aina yao ya uchezaji.
Mbappe pia aliwalaumu wachezaji wenzake hasa walipofanya kosa na Hispania wakafanikiwa kuupata mpira na hata ilipotokea wakaupata bado hawakuwa katika ubora na hilo likasababisha wafungwe.
Deschamps ambaye ameachana na Ufaransa, ni mchezaji wa zamani wa timu hiyo iliyobeba Kombe la Dunia mwaka 1998, akiwa kocha pia ameweka rekodi kwa kubeba Kombe la Dunia na timu hiyo mwaka 2018.
Nafasi ya Deschamps inatajwa kuchukuliwa na Zinedine Zidane au Zizou, mchezaji mwenzake wa zamani ambaye walikuwa pamoja katika kikosi cha Ufaransa kilichobeba Kombe la Dunia mwaka 1998.
