Rio de Janeiro, Brazil
Mshambuliaji wa timu ya taifa ya Brazil, Vinícius Junior ‘Vini Jr’ amewaomba radhi mashabiki wa timu hiyo baada ya kutolewa na Norway kwenye fainali za Kombe la Dunia 2026 hatua ya 16 bora.
Umahiri na ubora wa mshambuliaji wa Man City, Erling Haaland ulitosha kuwatoa mashindanoni, Brazil wakiwa chini ya kocha mkongwe, Carlo Ancelotti.
Brazil imeingia katika mechi hiyo ikiwa na tatizo la mastaa wake wa safu ya ushambuliaji kuwa majeruhi kina Rodrigo na Estevao huku mastaa wengine kina Raphinha na Lucas Paqueta kukwama mapema.
Inaaminika kuwa hali hiyo ilimuweka katika wakati mgumu Vinicius akiaminiwa kuipa mafanikio Brazil lakini aliishia kuifungia mabao manne na kutoa asisti moja katika mechi tano za timu hiyo.
“Ni takriban miaka minne baadaye najikuta katika kufikiria nini cha kuandika kwa mara nyingine baada ya mambo kuwa mabaya kwenye fainali za Kombe la Dunia,” alisema Vini.
Vini alisema kuwa amekuwa akiwaona watu wengi wa rika tofauti wakimuunga mkono na kushikamana na ndoto yao na isingekuwa sahihi kwake kukaa kimya ingawa alihitaji siku kadhaa za kutafakari.
Alisema kwamba kuvaa jezi ya timu ya taifa ni jambo kubwa na la kujivunia katika maisha yake na kutolewa katika fainali za Kombe la Dunia katika hatua ya 16 bora ni jambo gumu kulielezea.
Kutolewa kwa Brazil katika fainali hizo hata hivyo hakujawa sababu ya viongozi wa shirikisho la soka nchini humo kubadili msimamo kuhusu kuendelea kufanya kazi na kocha Carlo Ancelotti.
Kwa mantiki hiyo, Ancelotti, kocha wa zamani wa Real Madrid na kocha wa kwanza wa kigeni kuinoa timu ya Brazil ataendelea kuwa na timu hiyo.
