Na mwandishi wetu
Klabu ya soka ya Yanga imemtambulisha, Manqoba Mngqithi kuwa kocha mkuu mpya wa timu hiyo ambaye anaanza rasmi kazi kwa ajili ya msimu mpya wa 2026-27.
Taarifa za Yanga kutambulisha kocha mpya zilianza kuonekana katika mitandao ya kijamii Jumamosi Julai 10, 2026 baada ya kuwapo fununu zikihusisha makocha kadhaa akiwamo aliyewahi kuwa kocha wa Simba, Fadlu Davids.
Manqoba, 55, anachukua nafasi ya Pedro Concalves aliyetimuliwa mwezi Machi, 2026 na nafasi yake kukaimiwa na Abdihamid Moalin ambaye aliiwezesha Yanga kulitetea taji la Ligi Kuu NBC msimu uliopita wa 2025-26.
Kocha huyo mpya ni jina maarufu ukanda wa Afrika hasa kwao Afrika Kusini ambapo ametamba kwa muda mrefu na kikosi cha Mamelodi Sundowns, moja ya timu zenye mafanikio barani Afrika.
Akiwa na timu hiyo aliiwezesha kutawala soka nchini Afrika Kusini kwa kubeba mataji kadhaa pamoja na kuonesha ushindani katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Timu nyingine ambazo Manqoba amewahi kuzinoa mbali na Mamelodi ni Moja United, Amazulu FC, University of KwaZulu-Natal, Chippa United na timu yake ya mwisho ni Golden Arrows.
Mtihani wa kwanza kwa kocha huyo mwenye leseni ya Uefa utakuwa Agosti 12, 2026, Yanga itakapoumana na mahasimu wao Simba katika mechi ya Ngao ya Jamii, mechi ambayo ni rasmi kwa ufunguzi wa Ligi Kuu NBC msimu wa 2026-27.
Kimataifa Yanga yatambulisha kocha mpya
Yanga yatambulisha kocha mpya
Read also
