Liverpool, England
Klabu ya Liverpool imetangaza kumfuta kazi aliyekuwa kocha wake, Arne Slot baada ya kuinoa timu hiyo kwa misimu miwili.
Slot, 47, kocha kutoka Uholanzi msimu uliopita wa 2024-25 aliiongoza vyema timu hiyo hadi kubeba taji la Ligi Kuu England lakini msimu wake wa pili wa 2025-26 umekuwa mgumu.
Liverpool imemaliza msimu ikiwa nafasi ya tano, nafasi ambayo haikuwafurahisha mabosi wa timu hiyo hadi kumtimua kocha huyo huku majina kadhaa yakianza kutajwa likiwamo la aliyekuwa kocha wa Bournemouth, Andoni Iraola.
Taarifa ya wamiliki wa klabu ya Liverpool, Fenway Sports Group (FSG) imeuelezea uamuzi wa kumfuta kazi Slot kuwa ni mgumu kutokana na mchango wake kwa muda ambao amekuwa na timu hiyo.
“Huu ni uamuzi mgumu kwetu kuufanya kwa kuzingatia mchango wa Arne katika klabu ya Liverpool, muda ambao amekuwa hapa umekuwa wa mafanikio na wenye maana kubwa kwetu pamoja na mashabiki,” ilieleza taarifa ya FSG.
FSG pia walimshukuru kocha huyo kwa kila alichokifanikisha na kueleza kuwa shukrani hizo hazitoshi kwa namna ambavyo amekuwa akiwajibika kwa kuzingatia maadili ya kazi, umakini na kiwango cha juu cha utaalam.
Mambo yote hayo kwa mujibu wa FSG yanaendena na mtazamo wao kuwa Slot alikuwa kiongozi katika eneo lake.
Katika taarifa hiyo, FSG pia walibainisha kuwa tangu mara ya kwanza kukutana na Slot na kuanza kufanya naye kazi walibaini wazi kwamba hakuwa tu mtu mwenye kukubali majukumu yake bali aliyakumbatia.
