Na mwandishi wetu
Uongozi wa Simba umemtangaza Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Hamisi Mwinjuma ‘MwanaFA’ kuwa mgeni rasmi katika mechi yao ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Vipers ya Uganda.
Simba imemtaja MwanaFA kuwa mgeni rasmi wa mechi hiyo itakayopigwa Jumanne ya wiki ijayo katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, ikiwa ni siku chache tangu ateuliwe katika wadhifa huo.
Akizungumza jjini Dar es Salaam leo Ahamisi, Meneja Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally amesema sababu ya kumpendekeza kiongozi huyo ni mapenzi ya dhati aliyokuwa nayo kwa Simba.
“Mgeni rasmi katika mchezo wetu dhidi ya Vipers, tumemwalika Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Hamis Mwinjuma aje kumuona Simba ikimpelekea moto Vipers, tunaamini atakuwa chachu ya ushindi katika mchezo huo,” alisema Ally.
Kuhusu maandalizi ya timu hiyo kuelekea mchezo huo, Ally ameeleza kuwa kikosi chao kimeingia kambini jana mchana na jioni kilitarajiwa kuanza mazoezi kujiandaa na mchezo huo ambao wameupa uzito mkubwa.
Alisema wanahitaji pointi tatu nyingine kama walivyofanya kwenye mechi ya awali iliyochezwa wiki iliyopita nchini Uganda na Simba kuibuka na ushindi wa bao 1-0.
Ally alisema lengo lao ni kujiweka katika mazingira mazuri ya kutinga robo fainali kutoka kwenye Kundi C ambalo linaongozwa na Raja Casablanca ya Morocco.
“Tulikwenda kufufukia Uganda, na kweli tumefufuka. Jumanne ni mechi ya marudiano, katika mechi hii tunakwenda kuamua hatma ya Simba kwenye michuano ya CAF. tukimpiga tutafikisha pointi sita na kuanza kuchungulia robo fainali,” alisema Ally.
Kuhusu ujio wa Vipers, Ally alisema timu hiyo inayoburuza mkia kwenye msimamo wa kundi hilo, itawasili nchini Jumatatu asubuhi huku waamuzi watakaochezesha mchezo huo wanaotoka Ethiopia wakitarajiwa kutua nchini Jumapili mchana.
Ameeleza kuwa kuelekea mchezo huo wamebadilisha mfumo wa kutembelea maeneo mbalimbali ya Dar es Salaam kwa ajili ya kuwahamasisha mashabiki wao kwenda uwanjani kuipa sapoti timu.
“Tumekuwa tukizunguka kwenye maeneo mbalimbali ya wazi tukiwa na kispika, kutangaza mechi yetu, mechi hii tumekuja na kitu cha tofauti na chenye mvuto zaidi, kinaitwa Wenye Nchi Beach Party ambayo tutaifanya Jumapili hii kwenye ufukwe wa Coco,” alisema.
“Mashabiki wote tutakutana pale na kutakuwa na burudani mbalimbali kutoka kwa wasanii wengi na tiketi za mchezo huo zitauzwa siku hiyo,” alisema Ally.
Tiketi za mchezo huo zimeanza kuuzwa, Sh 3,000 kwa mzunguko, Sh 10,000 VIP C wakati Sh 20,000 ni VIP B huku Sh 30,000 ikiwa ni VIP A na Sh 150,000 kwa Platinum.
Sambamba na tiketi hizo, pia kutakuwa na tiketi za Simba Executive kwa ajili ya wateja wa Simba walio maofisini, faida zake ni kupata kibali cha kupelekwa uwanjani na basi na kukaa eneo maalumu na kupata huduma ya vinywaji baridi wakiwa uwanjani.
Soka MwanaFA mgeni rasmi, Simba-Vipers
MwanaFA mgeni rasmi, Simba-Vipers
Read also
