Na mwandishi wetu
Yanga imefuzu hatua ya fainali ya michuano ya Ngao ya Jamii baada ya kuwachapa mahasimu wao Simba bao 1-0 katika mechi iliyopigwa leo Alhamisi kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam.
Bao hilo pekee lililoipa ushindi Yanga katika mechi hiyo maarufu Dar au Kariakoo Derby lilipatikana dakika ya 44 mfungaji akiwa Maxi Nzengeli aliyetengewa mpira na Prince Dube.
Mpira uliozaa bao ulianzia kwa Duke Abuya aliyempasia kiungo mwenzake Pacome Zouazoua ambaye naye alipenyeza pasi ya chini chini kwa Dube.
Dube baada ya mpira huo kumfikia ilidhaniwa angepiga shuti la moja kwa moja lakini akamtengea mfungaji aliyefumua shuti la chinichini lililopita kwenye miguu ya kipa wa Yanga, Mussa Camara.
Simba ndio walioianza mechi kwa kasi na katika dakika ya kwanza tu Shomari Kapombe aliambaa na mpira upande wake wa kulia na kupiga krosi ya chinichini ambayo kama si umakini wa safu ya ulinzi ya Yanga chini ya kipa Djugui Diarra ubao ungesoma vingine.
Yanga nao wakajibu mapigo dakika moja baadaye kwa Pacome kumuunganishia pasi Dube ambaye shuti alilolipiga licha ya kumpita kipa wa Yanga lakini liligonga mwamba.
Timu hizo mahasimu ziliendelea kushambuliana kwa zamu na kuonesha kandanda safi kabla ya Yanga kupata bao hilo pekee na kwenda mapumziko wakiwa kifua mbele.
Kipindi cha pili timu zote zilikianza kwa kufanya mabadiliko ambapo Yanga iliwatoa Dube na kumuingiza Clement Mzize wakati Simba ilimtoa Muzamir Yassin na kumuingiza Valentine.
Mabadiliko ya wachezaji yaliendelea kwa Yanga kuwatoa Abuya, Aziz Ki na Pacome na nafasi zao kuingia Mudathir, Clatous Chama na Musonda wakati Simba nao iliwaingiza Kibu Dennis na Donaldo Ngoma badala ya Mukwale na Deborah Fernandez.

Matokeo hayo yanakuwa faraja kwa Yanga katika michuano ya Ngao ya Jamii baada ya mambo kuwa mabaya kwao mwaka 2023 ilipolala kwa penalti 3-1 mbele ya Simba baada ya sare ya 0-0.
Katika mechi nyingine ya Ngao ya Jamii iliyopigwa mapema hii leo kwenye Uwanja wa Amaan Zanzibar, Azam FC iliichapa Coastal Union mabao 5-2.
Baada ya matokeo hayo, Yanga na Azam zitaumana Agosti ili kumpata mshindi wa Ngao ya Jamii, michuano inayoashiria kuanza kwa msimu mpya wa soka la Tanzania.
