Na mwandishi wetu
Kocha Mkuu wa Azam FC, Youssouf Dabo (pichani) amewashauri mashabiki wa soka nchini kuacha mihemko ya kushinikiza kocha kufukuzwa pindi timu husika inapopata matokeo mabaya.
Baadhi ya mashabiki nchini walimtabiria kocha huyo kufutwa kazi kabla ya siku ya maadhimisho ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere kutokana na timu hiyo kuwa na mwenendo usioridhisha pamoja na kutolewa katika hatua ya awali kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika.
“Nilichogundua tangu nimekuja hapa ni mashabiki wa Tanzania wanazipenda timu zao zifanye vizuri, naheshimu hilo lakini siku zote mimi huwa sifanyi kazi kwa presha sababu naamini katika uwezo wangu na kingine bosi wangu ni mtu makini na amenihakikishia kuendelea kuwepo hapa kufikia malengo yetu,” alisema Dabo.
Kocha huyo alisema ukiacha kutolewa mapema kwenye Kombe la Shirikisho Afrika, bado ana imani ya kubeba ubingwa wa Ligi Kuu NBC msimu huu na hiyo ni kutokana na mwenendo mzuri wanaokwenda nao kwenye ligi hadi sasa.
Alisema katika mechi tano ambazo wamecheza hawajapoteza hata mchezo mmoja zaidi ya sare moja na kushinda michezo minne na kukaa nafasi ya pili kwenye msimamo.
Kocha huyo raia wa Senegal alisema kauli hizo za mashabiki anazichukulia kama changamoto zinazompa ari ya kuendelea kupambana na kutimiza malengo ya timu kama ambavyo wamekubaliana na uongozi wa timu hiyo yenye maskani yake Chamazi, Dar es Salaam.
