Barcelona, Hispania
Klabu ya Barcelona imemsajili mshambuliaji Vitor Roque (pichani) mwenye umri wa miaka 18 kutoka klabu ya Athletico-PR ya Brazil kwa ada ya Dola 44 milioni na mkataba utakaofikia ukomo msimu wa 2030-31.
Roque ambaye atajiunga na miamba hiyo ya Hispania majira ya kiangazi msimu ujao unakuwa ni usajili wa tatu katika klabu hiyo akiwa ametanguliwa na Ilkay Gundogan kutoka Man City na Inigo Martinez aliyekuwa Athletic Bilbao.
Inaaminika kuwa usajili wa Roque ni kama maandalizi ya kumpata msaidizi wa Robert Lewandowski ambaye Agosti atafikisha miaka 35 na hivyo lolote linaweza kumkuta kutokana na umri kuanza kumtupa mkono.
Barca baada ya kubaini kipaji cha Roque ilianza taratibu mazungumzo ya kumsajili, mazungumzo yaliyoongozwa vyema na Deco ambaye kwa sasa ndiye mkurugenzi wa michezo wa klabu hiyo.
Roque alionekana katika mechi kadhaa za Athletico pamoja na timu za vijana za Brazil, aliiwezesha Athletico kufikia hatua ya fainali ya michuano ya Copa Libertadores msimu uliopita na hivi karibuni aliitwa katika kikosi cha wakubwa cha timu ya Taifa ya Brazil.
Katika mechi 65 alizoichezea Athletico, Roque amefunga mabao 22 lakini la kuvutia zaidi ni mabao sita aliyoyafunga katika mechi sita zilizopita jambo ambalo limezidi kudhihirisha ubora wake katika kuzifumania nyavu.
Rais wa Barca, Joan Laporta alimpamba mchezaji huyo kutokana na namna anavyomudu kuitumia vyema miguu yote miwili jambo ambalo linamtofautisha na washambuliaji wengine wa Brazil.
“Ana staili ya kipekee, huwezi kumlinganisha na Ronaldo au Romario (washambuliaji wa zamani wa Brazil) huyu yeye ni mtu hatari kwa miguu yote anapokuwa ndani ya boksi, ni kijana, ana nguvu, na ni Mbrazil,” alisema Laporta.
Kimataifa Dogo wa Brazil asaini Barca
Dogo wa Brazil asaini Barca
Read also
