Istanbul, Uturuki
Kwa mara ya kwanza Man City imeshinda mataji matatu ‘treble’ msimu mmoja hapo hapo ikiweka rekodi nyingine ya kubeba kwa mara ya kwanza katika historia ya klabu hiyo taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Mafanikio hayo yamekuja baada ya Man City kuichapa Inter Milan bao 1-0 Jumamosi hii usiku katika mechi ya fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya iliyopigwa kwenye dimba la Ataturk mjini Istanbul, Uturuki.
Kwa mafanikio hayo, kocha Pep Guardiola na wachezaji wake wanakuwa wametimiza ndoto ya muda mrefu ya kutaka kubeba taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya pamoja na kubeba mataji matatu msimu mmoja.
Man City sasa wamehifadhi kabatini mataji ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, Ligi Kuu England (EPL) na Kombe la FA na hivyo kuwa timu ya kwanza kufanya hivyo tangu majirani zao Man United wafanye hivyo mwaka 1999 chini ya kocha Sir Alex Ferguson.
Ushindi wa taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya ambao umepatikana kwa bao la dakika ya 68 lililofungwa na Rodri pia unamfanya Pep aweke rekodi ya kubeba taji hilo mara tatu, alifanya hivyo mara mbili mwaka 2009 na 2011 akiwa kocha wa Barcelona.

Ndoto ya kutwaa mataji matatu ilikuwa ikimtesa Pep na wachezaji wake kwa muda mrefu lakini alikataa kuizungumzia kabla ya kuibuka na kutamka waziwazi mara baada ya kuipiku Arsenal katika EPL na kuwataka wachezaji wake waanze kupiga hesabu za mataji matatu.
Man City wana kila sababu ya kufurahia taji hilo hasa baada ya kulisotea kwa muda mrefu lakini kumbukumbu mbaya ya mwisho ni ile ya 2021 walipofikia hatua ya fainali lakini wakashindwa kutamba mbele ya Chelsea.
Kwa Pep kumekuwapo na hadithi ya muda mrefu kwamba ubora wake ungezungumzwa iwapo angeipa Man City taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya, na kwa sasa mjadala huo umezikwa rasmi baada ya kulibeba taji hilo na kuiingiza klabu hiyo katika rekodi ya kihistoria ya mafanikio barani Ulaya.
