Na mwandishi wetu
Kocha msaidizi wa Taifa Stars, Hemed Morocco amesema wamejiridhisha juu ya utimamu wa kimwili wa Feisal Salum ‘Fei Toto’ na mahitaji ya falsafa ya timu hiyo ndiyo maana wamemjumuisha kikosini.
Morocco ameeleza hayo baada ya kuibuka maswali juu ya kujumuishwa kwa kiungo huyo ambaye hajacheza kwa takriban miezi mitatu kutokana na mgogoro na waajiri wake, Yanga.
Feisal amekuwa kwenye mashauri ya kuvunja mkataba wake na Yanga kwa muda wote huo, hali inayompelekea kutoshiriki mashindano yoyote licha ya Yanga kuwa tayari kumpokea kuendelea na majukumu yake.
Morocco alifafanua kuwa uamuzi huo umefanyika kutokana na umuhimu wa kuipigania nchi katika mechi mbili zinazofuata za kufuzu Kombe la Mataia Afrika ‘Afcon’ 2023 dhidi ya Uganda lakini pia amejumuishwa kulingana na falsafa watakayokwenda kuitumia chini ya kocha mpya, Adel Amrouche.
“Fei tumemjumuisha kwa sababu licha ya kutocheza lakini anaonekana anafanya mazoezi, yuko vizuri na hili ni suala la kuipambania nchi, ukiwa mchezaji mzuri hata kama una mtatizo mengine, tutakuita.
“Niseme falsafa yetu pia imeona Fei atatusaidia, ni mdogo kwanza na tunawapenda wachezaji wa aina hii, hata kama hawapo kwenye mechi za ushindani, muhimu wanafanya mazoezi na tumejiridhisha na hilo, kwa hiyo tumemjumuisha tukiamini kitaifa ana kitu cha kutupa,” alisema Morocco.
Stars ambayo imeita kikosi cha wachezaji 31, inatarajiwa kuanza kuumana na Uganda ugenini nchini Misri Machi 24 kabla ya mechi ya marudiano itakayopigwa Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam Machi 28, mwaka huu.
