Na mwandishi wetu
Bao pekee la Depu limeiwezesha Yanga kunyakua pointi tatu muhimu katika mechi ya Ligi Kuu NBC dhidi ya Prisons, mechi iliyopigwa Alhamisi, Machi 12 2026 kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma.
Haikuwa rahisi kwa Yanga kupata bao hilo badala yake walihitaji dakika 79 za kupambana ndipo Laurindo Aurélio au Depu alipofunga bao hilo baada ya kipa wa Prisons, Mussa Mbisa kushindwa kuokoa mpira wa adhabu uliopigwa na Alan Okelo.
Mbisa awali aliuzuia mpira huo lakini ulirudi uwanjani na ndipo Depu alipoiwahi na kupata bao lililoamsha shangwe za mashabiki wa Yanga ambao walionekana kuanza kukata tamaa.
Prisons kwa muda mrefu wa mchezo huo ni kama vile waliingia uwanjani kwa lengo la kuizuia Yanga isipate bao mpango ambao ulionekana kuzaa matunda kwa kipindi chote cha kwanza kabla mambo hayajawaendea kombo dakika ya 79.
Ushindi huo unazidi kuiimarisha Yanga kileleni mwa msimamo wa ligi hiyo na sasa inakuwa imefikisha pointi 35 katika mechi 13 ikifuatiwa na JKT Tanzania inayoshika nafasi ya pili ikiwa na pointi 27.
Ligi hiyo inaendelea Ijumaa Machi 13, 2026 kwa mechi kati ya Mashujaa watakaokuwa wenyeji wa Fountain Gate kwenye Uwanja wa Lake Tanganyika mjini Kigoma.
Kimataifa Bao la Depu laibeba Yanga
Bao la Depu laibeba Yanga
Read also
