Rabat, Morocco
Timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars imetoka sare ya bao 1-1 na Uganda Cranes katika mechi ya Kundi C ya fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon 2025) iliyochezwa leo Jumamosi, Desemba 27, 2025.
Stars ndio waliokuwa wa kwanza kupata bao dakika ya 59 kwa mkwaju wa penalti uliopigwa na Simon Msuva na kumshinda kipa mkongwe wa Cranes, Dennis Onyango.
Penalti hiyo ilitolewa na mwamuzi baada ya Baba Alhassan wa Cranes, kuunawa mpira uliopigwa na Alphonce Mabula na Alhassan kujichanganya katika harakati za kuokoa na kujikuta akiuzuia mpira huo kwa mkono ingawa kipa wake aliokoa.
Cranes baada ya kufungwa bao hilo walianza kulisakama lango la Stars mara kwa mara huku Stars wakiwa na kazi ya kuzuia kabla ya mambo kuharibika dakika ya 69 baada ya Cranes kupata bao la kusawazisha.
Bao hilo lilitokana na mpira ulioanzia kwa kipa Onyango aliyetoa pasi ndefu kabla ya kupigwa krosi ambayo ilipigwa na Denis Omedi na Uche Ikpeazu akaujaza mpira wavuni kwa kichwa.
Kuingia kwa bao hilo ni kama vile kuliwaamsha Cranes ambao dakika chache baadaye nusura waandike bao la pili baada ya kupata penalti iliyotokana na makosa ya Haji Mnoga aliyemshika mchezaji mmoja wa Cranes lakini mpigaji wa penalti, Allan Okelo akaupaisha mpira.
Cranes ndio waliouanza mpira kwa kasi kwa kupeleka mashambulizi ya mapema yaliyoanzia kwa beki wa kushoto Abdul Aziz Kayondo ambaye alikuwa akipanda na kupiga krosi chonganishi ambazo hata hivyo ziliokolewa na kipa Zubeir Foba.
Stars nao walijibu mapigo na kutengeneza nafasi kadhaa ikiwamo dakika ya 41 baada ya Kelvin John akiwa katika nafasi nzuri lakini mpira alioupiga ulipaa juu ya lango la Cranes.

Katika mechi ya leo, kocha wa Stars Miguel Gamondi alianza kwa kumuweka benchi nahodha Mbwana Samatta kabla ya kumuingiza dakika ya 63 akichukua nafasi ya Kelvin John.
Mechi ya leo ilikuwa na neema mara mbili kwa Msuva kwani licha ya kufunga bao lililoibeba Stars pia ndiye aliyetajwa kuwa mchezaji bora wa mechi hiyo.
Kwa matokeo hayo, Stars na Cranes ambazo zimepangwa kundi moja na timu za Nigeria na Tunisia, sasa zitakuwa na kazi ya kuhakikisha zinashinda mechi zao za mwisho zilizobaki ili kufufua matumaini ya kusonga mbele hatua ya mtoano (16 bora).
Timu hizo zimepoteza mechi zao za kwanza, Stars ikilala kwa Nigeria na Cranes mbele ya Tunisia na katika mechi zao za mwisho hatua ya makundi zitakazochezwa Jumanne Desemba 30, 2025, Stars itaivaa Tunisia na Cranes itaumana na Nigeria.
