Monacxo, Ufaransa
Kiungo wa timu ya Monaco, Paul Pogba anajiandaa kucheza mechi ya kwanza akiwa na timu hiyo baada ya kuwa nje ya soka kwa kipindi kirefu kutokana na adhabu aliyopewa kwa kosa la kutumia dawa za kuongeza nguvu.
Pogba, 32, alijiunga na Monaco, timu ya Ligi 1 ya Ufaransa kipindi cha majira ya kiangazi mwaka jana baada ya adhabu aliyokuwa akikabiliwa nayo ya kufungiwa miaka minne kupunguzwa na Mahakama ya Kimataifa ya Michezo (CAS) hadi miezi 19.
Nyota huyo wa zamani wa timu ya taifa ya Ufaransa iliyobeba Kombe la Dunia mwaka 2018 aliingia katika kashfa ya utumiaji dawa za kuongeza nguvu hali iliyomfanya apotee kwenye soka na kudhaniwa kwamba huo ungekuwa mwisho wake.
Pogba ambaye pia amewahi kuichezea Man United, mara ya mwisho alionekana kwenye soka la ushindani, Septemba 2023 wakati huo akiichezea Juventus kwenye mechi ya Serie A dhidi ya Empoli.
Klabu ya Monaco ilimpa muda wa kufanya mazoezi kujiweka fiti na alitarajiwa kuanza kuichezea timu hiyo mapema mwezi huu kabla ya kupatwa na matatizo ya enka yaliyomuweka kando lakini kwa sasa jina lake limo katika orodha ya wachezaji wa Monaco ambao leo Jumamosi Novemba 22, 2025 watakabiliana na Rennes.
Baada ya kufanyiwa vipimo Agosti 2023, Pogba alikutwa na hatia na Februari 2024 alipewa adhabu ya kufungiwa miaka minne ingawa mwenyewe alidai kuna kosa lilifanyika alipopewa kilichoitwa dawa za kuongeza nguvu wakati nia haikuwa hiyo.
Moja ya kumbukumbu za Pogba kwa mashabiki wa Ufaransa ni siku alipofunga bao wakati Ufaransa ikiilaza Croatia 4-2 katika mechi ya fainal ya Kombe la Dunia 2018 nchini Ufaransa.
Kimataifa Pogba kurejea dimbani
Pogba kurejea dimbani
Read also
