Na mwandishi wetu
Simba imepata matokeo yasiyo ya kuvutia ya sare ya bao 1-1 dhidi ya Gaborone United ya Botswana ingawa imesonga mbele katika hatua ya pili ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa ushindi wa jumla wa mabao 2-1.
Katika mechi hiyo iliyochezwa leo Jumapili, Septemba 28, 2025 kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam, timu hiyo ambayo kwa sasa inanolewa na kocha wa timu ya taifa ya Tanzania, Hemed Suleiman Morocco baada ya kuondoka kwa Fadlu Davids ina kazi ya kufanya baada ya ushindi huo.
Ushindi wa Simba wazi umewaacha katika hali ya mshangao mashabiki wa timu hiyo ambao kwa sasa wanajiuliza kuhusu muelekeo wa timu hiyo ambayo msimu uliopita ilifikia hatua ya fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Katika mechi ya leo Simba ndio waliokuwa wa kwanza kupata bao dakika mbili kabla ya mapumziko mfungaji akiwa Jean Ahoua aliyeujaza mpira wavuni kwa mkwaju wa penalti iliyotolewa baada ya Morice Abraham kuangushwa katika eneo la penalti.
Gaborone walisawazisha bao hilo dakika ya 66 pia kwa mkwaju wa penalti uliojazwa wavuni na Lebogang Litsele, penalti iliyotolewa baada ya winga wa timu hiyo Thabo Maponda kuangushwa na Chamou Karaboue katika eneo la penalti.
Ukiacha mabao hayo timu zote zilipata nafasi kadhaa kutokana na mashambulizi yaliyotengenezwa lakini hadi dakika za 90 zinatimia hakuna timu iliyoweza kuongeza bao la pili.
Simba sasa inajiandaa kucheza hatua inayofuata ya michuano hiyo dhidi ya Nsingizini Hotspur ya Eswatini ambayo imesonga mbele kwa kuitoa Simba Bhora ya Zimbabwe kwa penalti 4-2, hiyo ni baada ya sare ya jumla ya bao 1-1 katika mechi zote mbili.
Kimataifa Simba yaitoa Gaborone United, yaacha maswali
Simba yaitoa Gaborone United, yaacha maswali
Read also
