Madrid, Hispania
Saa chache baada ya Olga Carmona kufunga bao lililoiwezesha Hispania kuilaza England 1-0 na kubeba Kombe la Dunia la Wanawake (WWC), Shirikisho la Soka Hispania (RFEF) lilimuarifu mchezaji huyo kuhusu kifo cha baba yake.
Olga, 23, (pichani),ambaye pia ni beki wa Real Madrid alifunga bao hilo dakika ya 29 na kuifanya timu ya wanawake ya Hispania iweke historia kwa kubeba taji hilo kwa mara ya kwanza.
Taarifa ya REEF ilieleza kuwa baba mzazi wa Carmona baada ya kuugua kwa muda mrefu hatimaye alifariki dunia Ijumaa wakati Hispania ilicheza na England mechi ya fainali juzi Jumapili.
“Tunasikitika kwamba tumelazimika kutangaza kifo cha baba wa Olga Carmona,” ilieleza taarifa ya RFEF ambayo pia ilichapishwa kwenye mitandao ya kijamii.
“Carmona alipata taarifa za kifo cha baba yake baada ya mechiya fainali ya Kombe la Dunia, tunatuma salamu za rambirambi kwa familia katika kipindi hiki cha huzuni. Tunakupenda Olga wewe ni sehemu ya historia ya soka la Hispania,” ilieleza taarifa hiyo ya REEF.
Mara baada ya filimbi ya kumaliza mchezo kupulizwa, wachezaji wa Hispania walianza kushangilia na kucheza uwanjani na Olga alionekana kuwa katika hali ya kawaida wakati wa makabidhiano ya kombe pamoja na medali.

Baadaye Olga alimzungumzia baba yake kupitia mitandao ya kijamii akisema kwamba hakuwa akijua kumbe kulikuwa na nyota yake iliyokuwa ikimuangazia kabla hata ya mechi kuanza.
“Najua ulinipa nguvu ya kufanikisha jambo la kipekee, najua utakuwa unaniangalia usiku huu na unajivunia mimi. Pumzika kwa amani Baba.” alisema Olga.
Klabu ya Real Madrid nayo ilituma salamu za rambirambi kwa familia ya Olga kufuatia kifo cha baba wa mchezaji huyo ambaye pia ndiye aliyefunga bao muhimu la Hispania katika mechi ya nusu fainali dhidi ya Sweden katika dakika ya 89.
