Sydney, Australia
Timu ya Wanawake ya Hispania imeibwaga England bao 1-0 na kubeba Kombe la Dunia la Wanawake (WWC) katika mechi ya fainali iliyopigwa Ijumaa hii mjini Sydney, Australia.
Alikuwa ni nahodha wa Hispania, Olga Carmona aliyefuta matumaini ya England katika dakika ya 29 baada ya kupachika bao hilo pekee akiyatumia makosa ya Lucy Bronze wa England aliyepoteza mpira katika eneo la kiungo.
Matokeo hayo yamewanyong’onyeza mashabiki wa England ambao kwa kipindi kirefu kabla ya mechi hiyo walikuwa wakiitambia timu yao wakiamini ina kila sababu ya kuweka historia kwa kubeba taji hilo kwa mara ya kwanza.
England ambao ndio mabingwa watetezi wa taji la Ulaya, waliamini huu ni wakati wao kupeleka taji jingine England baada ya lile la Ulaya lakini yote hayo yamezimwa baada ya timu hiyo kushindwa kutamba mbele ya Hispania.
Tangu timu ya wanaume ya England ibebe taji la Dunia mwaka 1966, si timu ya wanawake wala ya wanaume iliyofanya hivyo kwa mara nyingine hivyo matumaini makubwa yakabaki kwa timu ya wanawake kuweka rekodi kama hiyo jambo ambalo limezimwa na Hispania.
Matokeo hayo pia ni maumivu mengine kwa kocha wa England, Sarina Wiegman ambaye kwa mara ya pili anapoteza mechi ya fainali ya Kombe la Dunia ingawa mwaka huu matumaini yalikuwa makubwa mno.
Mara baada ya filimbi ya kumaliza mchezo kupulizwa, wachezaji wa England walionekana wakiwa na huzuni, wengi wao walianguka chini wakilia wakati kwa wenzao wa Hispania ilikuwa sherehe isiyo kifani.
Kipa wa England, Mary Earps alikoa michomo mingi iliyoelekezwa langoni mwake ikiwamo penalti ambayo Hispania walipewa katika kipindi cha pili baada ya kiungo wa England, Keira Walsh kuunawa mpira katika eneo la hatari lakini Earps aliokoa shuti lililopigwa na Jenni Hormoso.
Earps hata hivyo ana la kujivunia kwa kuwa nyota wa mchezo wa fainali lakini pia ndiye aliyetwaa tuzo ya Golden Glove kutokana na umahiri aliouonesha katika michuano hiyo.
Timu ya wanawake ya Hispania awali haikupewa nafasi yoyote ya kufikia hatua iliyofikia baada ya kuwapo mzozo baina ya wachezaji na viongozi wa Shirikisho la Soka la Hispania lakini hatimaye imeweka rekodi kwa kubeba taji hilo kwa mara ya kwanza.
Mzozo huo ulimuweka katika wakati mgumu kocha wa timu hiyo, Jorge Vilda na mapema akajikuta akiwakosa wachezaji Mapi Leon, Sandra Panos, Claudia Pina na Patri Guijarro ambao ndio walioisaidia Barcelona kubeba taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa wanawake mwezi Juni mwaka huu.
Katika mechi ya kusaka nafasi ya tatu iliyochezwa Jumamosi, Sweden walifanikiwa kuibuka vinara kwa kuwachapa wenyeji Australia mabao 2-0.
Kombe la Dunia Hispania yabeba Kombe la Dunia
Hispania yabeba Kombe la Dunia
Read also
