Na mwandishi wetu
Mechi ya Ligi Kuu ya Wanawake (TWPL) kati ya Simba Queens na JKT Queens imeshindwa kufanyika Jumanne hii baada ya kutokea utata wa viwanja kwa kila timu kwenda kwenye uwanja tofauti.
Simba Queens pamoja na waamuzi na maofisa wa mechi hiyo wao walikuwa Azam Complex wakati wapinzani wao walikuwa Mbweni kwenye dimba la Jenerali Isamhuyo wakiamini mechi ingechezwa kwenye uwanja huo.
Kwenye dimba la Chamazi baada ya waamuzi kuona timu pinzani haijafika walifuata taratibu husika na kumaliza mchezo kwa maana ya kwamba JKT Queens wameshindwa kufika uwanjani.
Wachezaji wa Simba Queens waliingia uwanjani kama kawaida na kufanya mazoezi mepesi tayari kwa kuwavaan JKT Queens ambao nao walikuwa Mbweni wakiwasubiri Simba Queens.
Mkanganyiko huo hata hivyo umepokewa kwa namna tofauti na JKT Queens ambao waliamini mechi hiyo ingechezwa kwenye dimba la Ismhuyo kama alivyonukuliwa ofisa habari wa timu hiyo, Masau Bwire akifafanua jambo hilo.

Kwa mujibu wa Bwire, ratiba ya mechi hiyo iliyotolewa na TFF ilionesha kwamba mechi hiyo ilipaswa kuchezwa kwenye dimba la Isamhuyo na habari ya Chamazi wameisikia wakati wakiwa uwanjani, kwa maana nyingine jambo hilo kwao ni geni.
Hapo hapo kuna taarifa kwamba mechi baina ya timu hizo ilifutwa hali ambayo inazidisha utata wa jambo hilo.
Wadau wengi wa soka wanasubiri kwa hamu kusikia TFF itaamua nini kuhusu mkanganyiko huo ambao kimsingi ni kama vile umesababishwa na ukosefu wa taarifa sahihi na kwa wakati sahihi.