Na mwandishi wetu
Ihefu FC imemtangaza Mecky Maxime kuwa kocha wao mkuu mpya kwa ajili ya kukinoa kikosi hicho chenye makazi yake Mbarali mkoani Mbeya.
Maxime ametangazwa na klabu hiyo leo Alhamisi ikiwa ni siku tano zimepita tangu aachane na Kagera Sugar kwa makubaliano ya pande zote mbili baada ya matokeo ya timu hiyo kuzidi kudorora.
Kwa mujibu wa taarifa ya Ihefu iliyowekwa kwenye mtandao wake, wanaamini Maxime ni kocha mzuri na mkubwa katika nchi hii, hivyo atawasaidia kufikia malengo waliyokusudia msimu huu.
“Maxime ni kocha mkubwa ndani ya nchi yetu na ni mzoefu kisoka kwa ngazi ya klabu na timu za taifa kwa ujumla, kuanzia sasa ataliongoza benchi letu la ufundi la Mbogo Maji kama kocha mkuu katika ligi na mashindano mengine,” ilieleza taarifa hiyo.
Maxime, mchezaji wa zamani wa Taifa Stars na timu ya Mtibwa Sugar, anatua Ihefu kuchukua mikoba ya kocha kutoka Uganda, Moses Basena aliyeoneshwa mlango wa kutokea mwanzoni mwa mwezi huu.
Kocha huyo mpya ana kazi kubwa ya kufanya kuiondosha timu hiyo kwenye nafasi za chini ambapo sasa inashika nafasi ya 13 ikiwa na pointi 13 baada ya michezo 14.