Manchester, England
Kocha wa Man United, Erik ten Hag amekanusha habari kwamba kuna mazungumzo yanaendelea ya mgomo katika timu hiyo na badala yake amesisitiza kwamba timu yake ipo katika njia sahihi.
Ten Hag amesema hayo baada ya ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Chelsea jana Jumatano katika Ligi Kuu England (EPL), huo ukiwa ushindi muhimu dhidi ya timu inayotajwa kuwa kubwa na ambao unaonekana kumpa nguvu kocha huyo.
Habari za kuwapo mgomo na sintofahamu katika kikosi hicho zilizidi kupata nguvu baada ya timu hiyo kupoteza mechi ya EPL dhidi ya Newcastle kwa bao 1-0.
“Mgogoro? Si kwetu, tumetulia, timu ipo katika njia sahihi, tulikuwa vizuri, wapambanaji na tuna furaha kwa hilo,” alisema Ten Hag.
Ushindi mbele ya Chelsea umekuwa na maana kubwa kwa Man United ambayo sasa imechupa hadi ‘top six’ kwenye EPL wakati mzunguko wa kwanza wa ligi hiyo ukielekea ukingoni.
Zaidi ya hilo, timu hiyo sasa imeachwa na Man City kwa tofauti ya pointi tatu tu jambo ambalo pia lina maana kubwa katika kuipa nguvu timu kuendelea kufanya vizuri.
Ten Hag hata hivyo pamoja na kuifurahia timu yake na kusisitiza kwamba ipo katika njia sahihi, amekiri kuwa bado kuna kazi kubwa ya kufanya.