Na mwandishi wetu
Mshambuliaji kinara wa Namungo, Realiants Lusajo amesema anapata hamasa kubwa kutokana na ushindani wa kuwania kiatu cha ufungaji bora msimu huu unaooneshwa na wachezaji Stephane Aziz Ki wa Yanga na Jean Baleke wa Simba.
Lusajo (pichani juu) ambaye jana alifunga bao lake la pili msimu huu walipoumana na Simba katika sare ya bao 1-1 amesema ushindani huo una afya na unamfanya apambane zaidi kuhakikisha anakimbizana na vinara hao ambao kila mmoja amefunga mabao saba.
“Binafsi huwa napenda mno timu yangu ipate inachokitaka kisha na mimi ndio nipate mafanikio binafsi lakini hakuna asiyependa kuwa mfungaji bora na ninafurahishwa na ushindani uliopo sasa kwa vinara wa mabao mpaka sasa.
“Msimu huu ushindani umekuwa wa mapema zaidi na unatia hamasa mno kwangu japo nimecheza mechi tano mpaka sasa lakini ushindani umekuwa mzuri na ligi imezidi kuimarika zaidi ya msimu uliopita, tutaendelea kupambana zaidi kuona tunaendelea kupata matokeo,” alisema Lusajo.
Mshambuliaji huyo aliyefunga mabao tisa msimu uliopita, alisema timu yao imeshindwa kufanya vizuri katika mechi za awali kutokana na sababu mbalimbali lakini sasa wanajipanga vilivyo kuhakikisha wanatoka nafasi ya 10 wakiwa na pointi nane na kuwania nafasi tano za juu kama ilivyo kawaida yao.