Na mwandishi wetu
Klabu ya Simba imeingia mkataba wa udhamini wa miaka mitatu na kampuni ya Serengeti Breweries Limited (SBL) kupitia kinywaji chake cha Pilsner Lager wenye thamani ya Sh bilioni 1.5.
Akizungumza Dar es Salaam leo Jumatano kwenye hafla fupi ya utiaji saini mikataba ya udhamini huo, Mtendaji Mkuu wa Simba, Imani Kajula alisema udhamini huo una maana kubwa kwa klabu kwani unaenda kuongeza chachu kwenye mapambano yao msimu huu katika michuano wanayoshiriki.
“Ni ubia wa nguvu kabisa wa wawili hawa. Hii ni nafasi ya kipekee ambayo imekuja wakati mwafaka. Serengeti ni mbia mkubwa sana wa mpira wa Tanzania, huu ni mwendelezo wa kusaidia mpira.
“Udhamini huu utasaidia uendeshaji wa klabu, gharama za uendeshaji wa vilabu huwa ni kubwa. Upatikanaji wa fedha ni muhimu sana. Tunawashukuru kukubali kuungana nasi kama wadhamini wa Simba.” alisema Kajula.
Mkurugenzi Mtendaji wa SBL, Obinna Anyalebechi alisema wanajivunia kuziunganisha taasisi mbili kubwa za SBL na Simba kwa mkataba wa udhamini huo ambao anaamini utakuza michezo nchini kwa namna moja ama nyingine.
Naye mjumbe wa bodi ya Simba, Raphael Chegeni, alisema hili ni tukio la kihistoria katika mechi zote ambazo Simba inacheza akiamini Pilsner Lager kuwa mshirika wa Simba hata mauzo yataongezeka.