Athens, Ugiriki
Vinara wa Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu wa 2022-23, Man City wameendeleza ubabe barani Ulaya kwa kubeba taji la Uefa Super Cup kwa kuibwaga Sevilla kwa penalti 5-4 baada ya sare ya bao 1-1.
Ushindi huo unaifanya Man City kuongeza taji la nne katika kipindi kisichozidi miezi sita, tayari ina mataji ya FA, Ligi Kuu England na Ligi ya Mabingwa Ulaya iliyoyabeba msimu uliopita wa 2022-23.
Katika mechi hiyo iliyopigwa mjini Athens Jumatano hii usiku, walikuwa ni Sevilla, vinara wa Europa Ligi waliondika bao la kwanza katika dakika ya 25 lililofungwa kwa kichwa na Youssef En-Nesyri.
Man City walisawazisha bao hilo kupitia kwa Cole Palmer ambaye aliinasa krosi iliyoanzia kwa Rodri katika dakika ya 63, bao lililozifanya timu hizo ziende kwenye mikwaju ya penalti.
Makipa wa Man City Ederson na Bono wa Sevilla walifanikiwa kuonesha umahiri wao kwa namna walivyookoa michomo mingi hadi kuzipeleka timu hizo kwenye mikwaju ya penalti.
Katika mikwaju ya penalti, jumla ya penalti tisa kati ya 10 zilizaa mabao, Nemanja Gudelj wa Sevilla ndiye mchezaji pekee aliyekosa penalti baada ya shuti lake kugonga mwamba.
Ushindi wa Man City pia unamfanya kocha wao, Pep Guardiola kuwa kocha wa kwanza kushinda taji la Uefa Super Cup na timu tatu za nchi tatu tofauti, alishabeba taji hilo pia akiwa Barcelona ya Hispania na Bayern Munich ya Ujerumani.
Kimataifa Man City vinara Uefa Super Cup
Man City vinara Uefa Super Cup
Read also